Maoni ya Prof. Haroub juu ya uanzishwaji wa ZIRPP

30 09 2009

Mohamed, nashukuru kwa kuja ofisini kwangu Zanzibar na kuniarifu juu ya azma ya kuanzisha ZIRPP, na kwa kutumiwa mjadala unaondolea juu ya suali hili. Kwa hakika nalifikiri yote ni kwa taarifa yangu mpaka pale uliponizinduwa tulipokutana pale mazikoni wiki iliyopita na kunitaka nichangie.

Kwanza ni jambo jema. Taasisi kama hiyo, na nyengine nyingi, inahitajika visiwani. Nakumbuka mwaka 1992, Dk Ahmed Gurnah wa Sheffield, Uingereza, alipokuja Zanzibar kwenye mkutano juu ya historia, alizungumza na baadhi yetu juu ya kuanzisha ‘Institute of Economic and Social Research’; na aliporejea aliandika ‘paper’ juu ya jambo hili na hata kuelezea kuwa alikuwa tayari kuchukuwa ‘early retirement’ ili kufanya shughuli hiyo.

Lakini kama ujuavyo, kila jambo na wakati wake. Na ule haukuwa wakati wake. Ingefaa ukamuomba akakutumia hiyo ‘paper’, labda itakupa mwangaza kidogo.

Kutokana na ‘inspiration’ ile tuliopata kutoka kwa Ahmed, mwaka jana mimi, Prof Issa Shivji na Prof Abdul Sheriff tumeanzisha ‘Zanzibar Indian Ocean Research Institute’ (ZIORI), makusudio yake yakiwa mapana kuliko yale aliyoyafikiria Ahmed na ambayo unayafikiria wewe. Ahmed tulimuomba na amekubali kuwa katika Bodi ya Washauri, wengine wakiwa wanatoka Kenya, Emirates, Malaysia, Canada, n.k.

Tulitoka ‘ukumbi’ Ogasti mwaka jana kwa kufanya mkutano mkubwa wa kimataifa Zanzibar ambao ulihudhuriwa na watu zaidi ya 150.

Makala zilizowasilishwa kwenye mkutano huo sasa zinahaririwa ili kutowa kitabu. Ukiangalia website ya ZIORI utaona nini madhumuni yake; au unaweza kutembelea ofisi zake pale nyuma ya SUZA na karibu na msikiti wa Seyyid Alawi.

Kutokana na uzoefu wangu wa kuongoza ‘Zanzibar Legal Services Centre’ kwa miaka 17 sasa napenda kukushauri kama ifuatavyo:

1. Kuna njia tatu za usajili: kama NGO, educational institution au company. Bahati mbaya NGO Act ina mapungufu mengi na ijapokuwa kumekuwa na ahadi kwa muda sasa kwamba itaangaliwa upya, hilo halionyeshi kwamba litafanyika leo au kesho. Kusajili kama educational institution kuna urasimu wake na madaraka makubwa anayo anaesajili. Ijapokuwa kusajili kama company ni rahisi kiurasimu, lakini baadhi ya wafadhili huwa hawapendelei kusaidia kitu kinachoitwa ‘company’. Kwa hivyo hao wataoandaa Katiba/Articles of Association wayajue haya.

2. Taasisi kama hii itahitaji iwe, na kwa mazingira ya kwetu, ionekane kuwa non-partisan, objective katika tafiti zake, na isiwe inafanya shughuli kwa kupendelea au kujipendekeza kwa mtu, kikundi au jumuiya yeyote ile.

Ili tafiti/maandishi/mapendekezo yake yakubalike itabidi wayatoayo hayo wawe ni watu wenye ujuzi katika fani zao na wanaoaminika kuwa wanaongozwa na ukweli.

3. Wataoongoza taasisi hiyo wawe ni watu waadilifu na wenye kuaminika na kukubalika kijamii na kitaaluma, na wataokuwa tayari kuwaongoza na kuwaendeleza vijana ili kizazi kipya kikuwe.

4. Taasisi kama hiyo ili ifanikishe malengo yake itahitaji misaada/michango ya kila aina na kutoka sehemu mbali mbali. Itabidi kwanza kuangalia kwamba misaada/michango haiitowi taasisi kutoka malengo yake; na kwamba kila kinachoingia kinatumiwa vizuri na kwa malengo yaliokusudiwa. Heshima ya taasisi na wale wanaohusika nayo inaweza kupotea kwa sababu ya ubadhirifu, uzembe, uchotaji na matumizi mabaya. Iwe marufuku kwa mtu kuitumia taasisi kwa manufaa yake. Zamani ilikuwa inawezekana ukigombana na SIDA ukakimbilia kwa DANIDA, au ukikosana na FNF ukaenda kwa FES.

Leo “with common European foreign policy”, ukikwaana na mmoja ndio umejichongea kwa wote.

Kwa leo nimalizie hapa. Nakutakia kila la kheri.


Actions

Information

Leave a comment