FAQs

MASUALA YAULIZWAYO MARA KWA MARA

Vipi Wazanzibari wanaweza kujiunga na ZIRPP?

Tungelipenda kujibu suala hili kwa kusema kuwa wanachotakiwa kufanya Wazanzibari ni kujaza fomu na kulipa ada zao za uwanachama kama baadhi yao walivyokwisha kufanya. Fomu za maombi zimeshatumwa kwa kupitia mialiko ya kujiunga na taasisi yetu iliyokuwa ikitolewa mara kwa mara. Ada ya uwanachama kwa Wazanzibari wanaoishi ndani ya Tanzania ni Tshs. 13,500/00 kwa mwaka; wakati Wazanzibari wanaoshi nje ya Tanzania wanalazimika kulipa ada ya USD 135.00 kwa mwaka. Kwa hivyo, kila anayetaka kujiunga na taasisi yetu yuko huru kuzijaza fomu hizo na kuzituma kwangu moja kwa moja kwa njia ya email.

ZIRPP imeweza kusajili wanachama wangapi mpaka hivi sasa tokea kuanzishwa kwake?

Hadi hivi sasa, ZIRPP imefanikiwa kusajili wanachama 100; kati ya wanachama hao, 80 ni Wazanzibari wanaoishi ndani ya Tanzania, na hasa zaidi Zanzibar; na 20 ni Wazanzibari wanaoshi nje ya Tanzania, wengi wao nchini Marekani. Kusudio kubwa la ZIRPP ni kusajili wanachama wengi zaidi wanaoishi katika nchi za nje; sio tu kwa madhumuni ya kukusanya fedha nyingi zaidi kutokana na michango ya ada za uwanachama, lakini zaidi kwa sababu Wazanzibari waishio nje ya Tanzania watapata fursa moja nzuri na muhimu sana ya kushiriki katika kuanzishwa kwa chombo kitakachowaunganisha na Wazanzibari wenzao walioko nchini kwa madhumuni ya kuchangia kwa hali na mali jitihada zao za pamoja za kujiletea maendeleo ya kweli na endelevu; na hasa zaidi kusaidia katika jitihada za kupunguza umasikini na kunyanyua hali za maisha yao.

ZIRPP imeweza kuchangisha kiasi gani cha fedha hadi hivi sasa?

Tokea zoezi la kusajili wanachama lianze mnamo mwezi wa Aprili 2009, jumla ya Tshs. 9,753,500/00 zimechangishwa kutoka kwa wanachama wa ZIRPP hadi hivi sasa. Kati ya hizo, Tshs 3,257,000/00 zimechangwa na Wazanzibari waishio nchini Tanzania; na Tshs. 6,496,500/00 (sawa na USD 4,997/00) zimechangwa na Wazanzibari waishio nje ya nchi. Kwa taarifa zaidi kuhusu ada za uwanachama na michango ya hiari kutoka kwa Wazanzibari mbali mbali, tafadhalini tembeleeni Weblog yetu: http://www.zirppo.wordpress.com.

Faida gani itapatikana kwa kujiunga na ZIRPP?

Hapa tungelipenda kusema kuwa faida kubwa itakayopatikana itatokana na ZIRPP kuzifanyia utafiti wa kina sera mbali mbali zinazobuniwa na kutekelezwa na serikali kwa madhumuni ya kuziboresha ili ziweze kutekelezeka kwa manufaa na faida ya wananchi kwa jumla. Kama mjuavyo, serikali imekuwa ikibuni sera na kuzipeleka haraka haraka katika Baraza la Wawakilishi ili kupitishwa bila ya kuzifanyia utafiti wa kina kwa madhumuni ya kujua faida zake na hasara zake. Kwa bahati mbaya, Wawakilishi wetu ambao wengi wao ni watu wenye elimu hafifu kidogo, wamekuwa wakizipitisha au kuziidhinisha sera hizo na kuzifanya kuwa sheria bila ya kutambua kwa undani athari zake (ziwe nzuri au mbaya) kwa jamii. Matokeo yake ni kudhoofika kwa uchumi wa nchi kutokana na utekelezaji wa sera mbovu, na hivyo kusababisha kuzorota kwa uchumi na maendeleo nchini.

Kwa mfano, nchini Marekani serikali inapotaka kuwasilisha Mswada wa Sheria katika Baraza la Wawakilishi (House of Representatives) au katika Baraza la Senate, rasimu ya Muswada huo, kabla ya kupelekwa katika mabaraza hayo, kwa kawaida huwa inatangazwa katika magazeti pamoja na vyombo vingine va habari ili kuwajuulisha wananchi kupitia taasisi zao mbali mbali, kwa madhumuni ya kuujadili Muswada huo, kuuchambua na kuutolea maoni. Mfano mzuri ni sera ya Huduma ya Afya na Muswada wake kama ulivyobuniwa na kupendekezwa na Rais Barack Obama hivi karibuni; Muswada ambao umebuniwa na kutayarishwa rasmi zaidi ya miezi mitano iliyopita. Wadau na wahusika mbali mbali wameujadili katika vikao mbali mbali na kuutolea maoni; mpaka hatimaye kupitishwa hivi majuzi tu katika Baraza la Wawakilishi la Marekani. Na hivi sasa Muswada huo umeshaanza kujadiliwa katika Baraza la Senate. La muhimu hapa ni kuwa Wamarekani, kwa ujumla wao, walipatiwa nafasi na muda wa kutosha kuujadili muswada huo kwa kina. Kwa bahati mbaya, utaratibu wa aina hii hauko kwetu. Matokeo yake, sera na miswada yake yote huwa inapitishwa bila ya mijadala ya kina; na hivyo kuzorotosha kupatikana kwa maendeleo ya kweli kwa maslahi na faida ya wananchi.

Kwa hivyo, kwa kuijunga na ZIRPP, Wazanzibari watapata chombo kimoja muhimu sana kitakachowasaidia kuondosha kasoro za aina hii na badala yake kuleta ufanisi mkubwa katika utendaji mzima wa shughuli za serikali; na hasa zaidi katika nyanja za ubunifu na utekelezaji wa sera mbali mbali za kijamii zinazobuniwa na kutekelezwa na serikali.

Nini hasa majukumu na malengo ya ZIRPP?

Majukumu na malengo makuu ya ZIRPP yameorodheshwa kwa uwazi na ufasaha mkubwa katika katiba yake. Lakini, kwa muhtasari tu, moja kati ya malengo yake muhimu ni kujaribu kadri itakavyowezekana kuondoa utaratibu wa kubuni na kutekeleza sera mbali mbali bila ya kutoa nafasi na muda wa kutosha kwa wananchi kupitia jumuiya zao mbali mbali kujadili sera zinazobuniwa na kutekelezwa kwa madhumuni ya kuzitolea maoni kabla ya kupitishwa na Baraza la Wawakilishi na kuwa sheria kamili. ZIRPP itafanya hivi kwa njia ya kuelimishana kupitia utafiti na kwa kutumia nguvu ya hoja kwa madhumuni ya kujaribu kuanzisha utamaduni mpya utakaokwenda sambamba na aina ya taratibu zinazotumika katika nchi zilizoendelea ili Wazanzibari nao wapatiwe nafasi na muda wa kutosha kushiriki kikamilifu katika mijadala ya sera mbalimbali zinazogusa maslahi na maisha yao ya kila siku. Baada ya kuzifanyia utafiti wa kina sera husika, ZIRPP itatoa ripoti kamili kuhusu utafiti uliofanywa kwa kuelezea kwa uwazi kabisa matokeo ya utafiti huo na kutoa mapendekezo kamili juu ya hatua za kuchukuliwa. Ripoti pamoja na mapendekezo hayo yatawasilishwa serikalini kwa madhumuni ya kuitaka serikali kuyatekeleza kadri itakavyowezekana. Katika tafiti zake, Mkakati wa Serikali katika Kupunguza Umasikini Zanzibar (MKUZA) utapewa kipaumbele maalumu.

Jee, ZIRPP imefungamana na chama gani cha kisiasa?

Kwa mujibu wa katiba yake, ZIRPP inapaswa kutokufungamana na chama chochote kile cha kisiasa. Kwa madhumuni ya kutetea na kulinda sera hii kikamilifu, ZIRPP haitolinda wala kutetea sera za chama chochote kile cha kisiasa; wala haitompigia debe au kumuunga mkono mgombea yoyote yule aliyesimamishwa na chama chochote kile cha kisiasa kugombea nafasi yoyote ile wakati wa chaguzi mbali mbali zinazoendeshwa nchini katika ngazi za wilaya, mkoa na kitaifa. Kwa lugha nyingine, ZIRPP itakuwa “neutral” kabisa katika nyanja zote za kisiasa; ingawaje katika kutekeleza majukumu yake, ZIRPP haitosita kuipongeza serikali kila pale inapoonekana kufanya vizuri katika kulinda na kutetea maslahi ya wananchi; na vile vile haitoogopa kuikosoa serikali kila pale inapoonekana kufanya vibaya kwa madhumuni ya kujenga zaidi kuliko kubomoa.

Fedha zilizochangishwa na wanachama ikiwa ni pamoja na Wazanzibari wengine kwa ajili ya kusaidia kuanzishwa kwa ZIRPP zimetumika vipi?

Kuhusu matumizi ya fedha zinazotokana na wanachama au wachangiaji wengine kwa ajili ya ZIRPP; sehemu kubwa ya fedha zilizochangishwa, kwa sasa, imetumika kwa ajili ya kulipia kodi ya Ofisi yetu kwa miezi sita; utiaji wa fanicha za ofisi; i.e. meza, viti, meza kubwa za mikutano pamoja na viti vyake na kuunganisha huduma za Fax na simu. Pamoja na matumizi yote hayo, bado Taasisi inahitaji fedha zaidi kwa ajili ya kununulia vitendea vyingine vya kazi, kama vile kompyuta za kutosha, video conference equipment, photo copy machine, printers, projectors, video cameras, Digital cameras, na TV sets kwa ajili ya kufanyia utafiti. Pia, tunahitaji fedha za kununulia sofa sets, carpets, stationaries pamoja na vifaa vyengine vingi vya ofisi.

Faida gani nyingine zitapatikana kwa kuanzishwa kwa ZIRPP?

Kwa hivyo, ikiwa ZIRPP itaanza kazi zake ipasavyo kama inavyotarajiwa, basi faida kubwa sana itapatikana kutokana na ukweli kuwa Zanzibar itakuwa imeanzisha taasisi ya kwanza kabisa katika historia yake yenye kujikita zaidi katika masuala ya utafiti wa sera za kijamii; taasisi ambayo itasaidia sana katika kuwafunua macho wananchi wa kawaida na hata Wabunge na Wawakilishi wa Kizanzibari kuelewa namna ya sera zinavyobuniwa na kutekelezwa na serikali kwa njia na utaratibu wa uwazi na ufanisi mkubwa. Kwa kupitia ZIRPP, serikali pamoja na wananchi wataweza kujifunza jinsi ya kupatikana kwa ufanisi katika ubunifu na utekelezaji wa sera mbali mbali kwa kutoa mifano mizuri inayohusiana na utekelezaji wa sera kama hizo katika nchi nyingine ili Zanzibar isirudiye makosa yanayoendelea kufanywa nchini siku hadi siku; na hivyo kusaidia sana katika kuleta maendeleo makubwa, endelevu na ya kweli kwa wananchi wake.

ZIRPP pia itaweza kutoa mchango mkubwa na muhimu sana kwa kuionesha serikali njia nzuri ya ubunifu na utekelezaji wa sera na kuitaka kuiga mifano mizuri inayofanyika kwengineko badala ya kutekeleza sera zisizofanyiwa utafiti wa kina kwa madhumuni ya kujua faida na hasara zake. Nchi nyingi, hasa zile zilizoendelea, kama vile Marekani, Ulaya Magharibi, na kule Asia, zimepiga hatua kubwa kiuchumi na kimaendeleo kutokana na kuwepo kwa jumuiya kama hizi; yaani think-tanks, ambazo zinasaidia sana kifikra na kimawazo katika jitihada za kupunguza umasikini na kusukuma maendeleo ya kweli na endelevu katika nchi husika.

Faida gani nyingine kubwa na muhimu zaidi inayoweza kupatikana kwa kuanzishwa kwa ZIRPP?

Faida kubwa zaidi itayoweza kupatikana kupitia ZIRPP itatokana na uwezekano wa kuwaunganisha Wazanzibari kuwa kitu kimoja popote pale walipo duniani bila ya kujali itikadi zao kisiasa, kijinsia, kidini, kirangi na kadhalika. Kwa lugha nyingine, Wazanzibari wataungana na kuachana na tofauti zao za kisiasa kwa misingi ya kujenga nchi yao zaidi kuliko kushabikia siasa za vyama vyao. Hii ni faida kubwa sana itakayoweza kupatikana ikiwa Wazanzibari wataiunga mkono Jumuiya yetu hii, ambayo ni ya kwanza kabisa katika historia ya nchi yetu, kwa hali na mali.

ZIRPP ina wafanya kazi wangapi?

Hadi hivi sasa, ZIRPP inaendeshwa na kuongozwa na wafanya kazi wawili (Kaimu Mkurugenzi Mtendaji na Kaimu Mshika Fedha) wa muda kwa njia ya hiari, kujitolea na bila ya malipo. Lakini, kutokana na haja iliyojitokeza baada ya kuhamia katika Ofisi yetu, ZIRPP imeajiri msafishaji wa Ofisi (cleaner); na inakusudia kuajiri Executive Assistant kwa madhumuni ya kutoa huduma za kiutawala (Administrative Support) kwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji na Kaimu Mshika Fedha. Pia, ZIRPP inakusudia kutumia kikamilifu huduma zitakazotolewa na wafanya kazi wengine wawili ambao wameelezea azma yao ya kutaka kuitumikia ZIRPP kwa njia ya hiari, kujitolea na bila ya malipo. Kaimu Mkurugenzi Mtendaji anakusudia kuwapangia kazi kwa mujibu wa taaluma zao katika wakati unaofaa.

Lini ZIRPP itaanza kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa katiba yake?

Hivi sasa uongozi wa ZIRPP umo mbioni katika jitihada za kukamilisha utayarishaji wa Mkakati wa Mpango wa Muda Mfupi (Strategic Medium-Term Plan) utakaoelezea kwa kina na ufasaha mkubwa programu, shughuli, malengo na majukumu ya Taasisi katika kipindi cha miaka minne ijayo; ikiwa ni pamoja na idadi ya wafanya kazi na mishahara yao, vitendea kazi na gharama zake zote. Mara tu baada ya kukamilika utayarishaji wa Mkakati huo, uongozi wa ZIRPP utaitisha Mkutano wa Baraza Kuu (General Assembly) utakaojumuisha wanachama wake wote kwa madhumuni ya kuchagua Wajumbe 13 wa Baraza la Utawala (Governing Council) ambalo litakuwa na jukumu, pamoja na mambo mengine, la kuujadili Mkakati huo na kuupitisha ikiwa ndio dira itakayoongoza shughuli za Taasisi kwa kipindi cha miaka minne ijayo. Mchakato huu unategemewa kufikia kilele chake mnamo mwisho wa mwezi wa Desemba na hivyo Taasisi kuanza kutekeleza majukumu yake ifikapo tarehe 1 Januari 2010 baada ya sherehe za uzinduzi rasmi..

MWISHO: Kama tulivyowahi kukueleza huko nyuma, hivi sasa ZIRPP inahitaji computers haraka kabisa. Hatuwezi tena kusubiri bila ya kikomo. Ikiwa kuna mtu yoyote mwenye computer moja au zaidi na anakusudia kuitoa kwa matumizi ya ZIRPP, basi tafadhali tunaomba atuarifu haraka ili tutafute namna ya kuzisafirisha kutoka huko aliko hadi Zanzibar. Hili sio jambo la kusubiri tena. We must act now. Tunatanguliza shukrani zetu za dhati kwenu kwa jitihada zenu za pamoja za kuisaidiya ZIRPP. Ahsanteni sana.

Muhammad Yussuf
INTERIM EXECUTIVE DIRECTOR

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s
%d bloggers like this: