Hali bado tete Pemba

16 09 2009

15th September 2009

Jeshi la Polisi Kisiwa cha Pemba limeanza kutumia maji ya kuwasha kutawanya mamia ya wananchi wanaopinga ubaguzi katika uandikishaji wapiga kura, huku shinikizo la kuzuia zoezi hilo likichukua sura mpya baada ya vyumba vya vituo vya kuandikisha wapigakura kumwagwa upupu.

Miongoni mwa vituo ambako upupu huo umemwagwa, ni pamoja na kwenye skuli ya Shumba Vyamboni, iliyoko katika Jimbo la Tumbe, Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Kutokana na kitendo hicho, zoezi la uandikishaji wapiga kura lilishindikana kufanyika baada ya maofisa wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kushindwa kuingia ndani ya vyumba hivyo.

Mkuu wa Kituo hicho, Juma Omari Yusufu, ambaye yeye na maofisa wa ZEC pamoja na vifaa vya kuandikisha wapiga kura walikutwa wakiwa nje ya kituo, alithibitisha upupu huo kumwagwa ndani ya vyumba hivyo.

“Vyumba haviingiliki, kumeingizwa upupu, tumepeleka ripoti kwa wakubwa, tunasubiri maamuzi,” alisema Yusufu.

Mbunge wa Konde, Dk Tarab Ali Tarab (CUF), ambaye ni miongoni mwa waangalizi wa zoezi hilo, alivimba sehemu mbalimbali za mwili wake ikiwamo mikono na uso kutokana na kuathiriwa na upupu huo.

Tangu juzi hakuna hata mtu mmoja aliyejiandikisha katika kituo hicho kutokana na wananchi kugomea zoezi hilo karibu kisiwa chote cha Pemba wakipinga wenzao kukataliwa kuandikishwa baada ya kunyimwa kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi (Zan ID).

Mkurugenzi wa ZEC, Salim Kassim Ali alipoulizwa jana kuhusu hatma ya zoezi hilo, aliahidi kuzungumzia suala hilo baadaye.

Tukio hilo lilitokea saa 6 mchana katika kituo cha Skuli ya Kambini Mchangamdogo, baada ya gari linalotumiwa na kiongozi huyo mmoja wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kisiwani kuwabeba watu hao na kuwapeleka kuandikishwa katika kituo hicho.

Katika tukio hilo, watu kadhaa walijeruhiwa kukimbizwa katika hospitali ya Wilaya ya Wete.

Mbali na hilo askari hao pia walifyatua mabomu ya machozi kuwatawanya wananchi waliokusanyika katika kituo cha Kiuyu Minungwini.

Wakati hayo yakijiri, vurugu kubwa ilitokea kisiwani hapa jana baada ya askari wa Kikosi cha Kuguliza Ghasia (FFU), kutumia maji hayo kuwatawanya wananchi waliojaribu kuwazuia baadhi yao kuandikishwa.

Nayo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), imesema imeshitushwa na vitendo vinavyoendelea kujitokeza kwa baadhi ya wananchi kugoma kujitokeza kuandikishwa katika daftari la kudumu la wapiga kura.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Kiongozi, Hamza Hassan Juma alitoa kauli hiyo jana baada ya kujitokeza vurugu katika vituo vya uandikishaji wapiga kura na kusababisha mamia ya wananchi kushindwa kujiandikisha katika Kisiwa cha Unguja na Pemba.

CHANZO: NIPASHE





SMZ yadai Marekani ina mkono vurugu za Z’bar

16 09 2009

Na Salma Said, Wete Pemba

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imedai fujo zinazoendelea hivi sasa
kisiwani Pemba ni mpango maalumu na wa muda mrefu wa serikali ya Marekani.

Kauli hiyo ya kulishutumu taifa kubwa duniani imetolewa na Waziri wa
Nchi Ofisi ya Waziri Kiongozi, Hamza Hassan Juma alipokuwa akizungumza
na waandishi wa habari jana nje ya kituo cha uandikishaji cha shule ya
Sizini mkoami Kaskazini Pemba.

Mwishoni mwa mwezi uliopita, Marekani ilitoa taarifa kwa raia wake
ikiwataka kuwa makini na safari za kisiwani Pemba ambako ilisema kuna
vurugu zinazohusiana na uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.

Marekani, ambayo ina tabia ya kutahadharisha raia wake kufanya ziara
sehemu ambazo kuna ama kunaweza kutokea vurugu, ilieleza kuwa tangu
kuanza kwa zoezi la uandikishaji wapiga kura, kumekuwa na vurugu kubwa
kisiwani Pemba na kuwaonya raia wake kuwa makini na mikusanyiko wawapo
visiwani Zanzibar, huku ikiwataka wajiandikishe kwenye ubalozi wake mara
watakapowasili Tanzania.

Lakini SMZ ilijibu vikali taarifa hiyo ya tahadhari kwa raia wa Marekani
na jana Waziri Juma alieleza msimamo wa serikali yake kuhusu kitendo
hicho cha Marekani.

“SMZ inaamini kwamba Marekani ilikuwa inajua nini kitatendeka katika
kisiwa cha Pemba na ndio maana ikaanza kutoa tahadhari kwa wananchi wake
mapema,” alisema Waziri Juma ambaye alisema ametumwa na serikali kwenda
Pemba kuangalia hali ya usalama.

“Haiwezekani Marekani iwatake wananchi wake wasitembelee kisiwa cha
Pemba halafu iwe haijui nini kitatokea katika kisiwa hicho.

“Sisi serikali ya Zanzibar tunaamini kwamba Marekani ndio iliyopanga
mpango huu maalumu wa kufanyika vurugu huku Pemba na ndio maana
wakawatahadharisha raia wake mapema wasitembelee Pemba. Kama walikuwa
hawajui kwa nini watoe tahadhari? Wanajua na ndio waliopanga mpango huu
kwa kutafuta sababu wanazozijua wao.”

Zoezi la uboreshaji wa daftari la wapiga kura kisiwani Zanzibar
limekumbwa na vurugu kubwa na awali serikali ililazimika kulisimamisha
baada ya wananchi kurushiana mawe na polisi. Juzi polisi walilazimika
kutumia silaha za moto kutawanya wananchi ambao walijikusanya nje ya
vituo vya kujiandikishia kwa lengo la kuzuia wenzao kujiandikisha.

Tayari nchi 14 wanachama wa Umoja wa Ulaya (EU) na Marekani zimeshaitaka
SMZ kushughulikia matatizo yaliyojitokeza kwenye zoezi la uandikishaji
wapigakura ili kuufanya uchaguzi ujao kuwa huru na wa haki. Tatizo kubwa
linalopingwa na wananchi wa Zanzibar ni matumizi ya kitambulisho cha
Mzanzibari Mkaazi kama ndio sifa kuu ya mtu kuandikishwa.

Wananchi wengi visiwani Zanzibar, ambako mkaazi ni yule aliyeishi kwa
miaka mitatu mfululizo, wanadai wamenyimwa vitambulisho vya ukaazi na
hivyo hawawezi kuandikishwa kupiga kura.

Waziri huyo pia alisema ili kuondokana na masharti ya nchi wahisani, SMZ
itaanza kusimamia uchaguzi wake na kuachana na ufadhili wa wahisani kwa
madai kuwa uzoefu unaonyesha kuwa ufadhili huambatana na masharti, jambo
ambalo alisema si jema.

Kwa mujibu wa Waziri Juma, pamoja na kuwa nchi wahisani wanatoa fedha
kwa ajili ya kusaidia miradi mbalimbali, hakuna sababu ya nchi hizo
kuingilia mambo ya ndani kwa kuwa kila nchi ina uhuru wake na inajiendesha.

Alisema fedha zinazochangwa na wafadhili ndio zinazosababisha matatizo
yanayototokea Pemba sasa kwa kuwa wafadhili huwa wana masharti yao,
hivyo SMZ itaanza kusimamia uchaguzi wake hata kama italazimika
kuchangishana shilingi moja moja.

Chanzo: Mwananchi