SMZ yadai Marekani ina mkono vurugu za Z’bar

16 09 2009

Na Salma Said, Wete Pemba

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imedai fujo zinazoendelea hivi sasa
kisiwani Pemba ni mpango maalumu na wa muda mrefu wa serikali ya Marekani.

Kauli hiyo ya kulishutumu taifa kubwa duniani imetolewa na Waziri wa
Nchi Ofisi ya Waziri Kiongozi, Hamza Hassan Juma alipokuwa akizungumza
na waandishi wa habari jana nje ya kituo cha uandikishaji cha shule ya
Sizini mkoami Kaskazini Pemba.

Mwishoni mwa mwezi uliopita, Marekani ilitoa taarifa kwa raia wake
ikiwataka kuwa makini na safari za kisiwani Pemba ambako ilisema kuna
vurugu zinazohusiana na uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.

Marekani, ambayo ina tabia ya kutahadharisha raia wake kufanya ziara
sehemu ambazo kuna ama kunaweza kutokea vurugu, ilieleza kuwa tangu
kuanza kwa zoezi la uandikishaji wapiga kura, kumekuwa na vurugu kubwa
kisiwani Pemba na kuwaonya raia wake kuwa makini na mikusanyiko wawapo
visiwani Zanzibar, huku ikiwataka wajiandikishe kwenye ubalozi wake mara
watakapowasili Tanzania.

Lakini SMZ ilijibu vikali taarifa hiyo ya tahadhari kwa raia wa Marekani
na jana Waziri Juma alieleza msimamo wa serikali yake kuhusu kitendo
hicho cha Marekani.

“SMZ inaamini kwamba Marekani ilikuwa inajua nini kitatendeka katika
kisiwa cha Pemba na ndio maana ikaanza kutoa tahadhari kwa wananchi wake
mapema,” alisema Waziri Juma ambaye alisema ametumwa na serikali kwenda
Pemba kuangalia hali ya usalama.

“Haiwezekani Marekani iwatake wananchi wake wasitembelee kisiwa cha
Pemba halafu iwe haijui nini kitatokea katika kisiwa hicho.

“Sisi serikali ya Zanzibar tunaamini kwamba Marekani ndio iliyopanga
mpango huu maalumu wa kufanyika vurugu huku Pemba na ndio maana
wakawatahadharisha raia wake mapema wasitembelee Pemba. Kama walikuwa
hawajui kwa nini watoe tahadhari? Wanajua na ndio waliopanga mpango huu
kwa kutafuta sababu wanazozijua wao.”

Zoezi la uboreshaji wa daftari la wapiga kura kisiwani Zanzibar
limekumbwa na vurugu kubwa na awali serikali ililazimika kulisimamisha
baada ya wananchi kurushiana mawe na polisi. Juzi polisi walilazimika
kutumia silaha za moto kutawanya wananchi ambao walijikusanya nje ya
vituo vya kujiandikishia kwa lengo la kuzuia wenzao kujiandikisha.

Tayari nchi 14 wanachama wa Umoja wa Ulaya (EU) na Marekani zimeshaitaka
SMZ kushughulikia matatizo yaliyojitokeza kwenye zoezi la uandikishaji
wapigakura ili kuufanya uchaguzi ujao kuwa huru na wa haki. Tatizo kubwa
linalopingwa na wananchi wa Zanzibar ni matumizi ya kitambulisho cha
Mzanzibari Mkaazi kama ndio sifa kuu ya mtu kuandikishwa.

Wananchi wengi visiwani Zanzibar, ambako mkaazi ni yule aliyeishi kwa
miaka mitatu mfululizo, wanadai wamenyimwa vitambulisho vya ukaazi na
hivyo hawawezi kuandikishwa kupiga kura.

Waziri huyo pia alisema ili kuondokana na masharti ya nchi wahisani, SMZ
itaanza kusimamia uchaguzi wake na kuachana na ufadhili wa wahisani kwa
madai kuwa uzoefu unaonyesha kuwa ufadhili huambatana na masharti, jambo
ambalo alisema si jema.

Kwa mujibu wa Waziri Juma, pamoja na kuwa nchi wahisani wanatoa fedha
kwa ajili ya kusaidia miradi mbalimbali, hakuna sababu ya nchi hizo
kuingilia mambo ya ndani kwa kuwa kila nchi ina uhuru wake na inajiendesha.

Alisema fedha zinazochangwa na wafadhili ndio zinazosababisha matatizo
yanayototokea Pemba sasa kwa kuwa wafadhili huwa wana masharti yao,
hivyo SMZ itaanza kusimamia uchaguzi wake hata kama italazimika
kuchangishana shilingi moja moja.

Chanzo: Mwananchi

Advertisements

Actions

Information

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s
%d bloggers like this: