Kutana na Chaap: “Tiger Woods” wa Zanzibar

25 02 2010

Na Talib Kassim Abdi

Kitu gani kilichomfanya Issa Mohammed Faki Mjaka akurubiane au awe na mawasiliano ya karibu na Wakoloni wa Kiingereza kama vile waliokuwa British Resident Sir George Mooring, Kamishna wa Polisi Biles, Kamishna wa Magereza Francis, Jaji Mkuu Horstfall, Jaji Mwandamizi Dulton, na Kamishna Mkuu wa Idara ya Upelelezi Speight katika serikali ya Kikoloni kabla ya Uhuru wa Zanzibar mnamo mwaka 1963 na Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964?

Jibu la suala hili ni rahisi kabisa kupatikana. Issa Mohammed Mjaka, ambaye ni maarufu kwa jina la Chaap, kama ilivyokuwa kwa watoto wengi wa rika lake waliokuwa wakiishi Kikwajuni, Mjini Zanzibar, katika miaka ya 1950 na 1960, alikuwa ni mmoja miongoni mwa vijana waliokuwa wakiwabebea Wakoloni hao mikoba yao iliyojaa vingowe vya kuchezea mmoja kati ya michezo maarufu duniani unaojuulikana kama ”Golf”. Vijana hawa walikuwa wakijuulikana kama ”Keddies”; kibarua ambacho kiliwapatia vijisenti kidogo vya kuwawezesha kukimu hali ngumu ya maisha wakati huo.

Issa Mohammed Faki Mjaka 'Chaap'

Wakati ule, kedi alikuwa analipwa jumla ya senti 75 kwa mzunguko mmoja wa vishimo 9; na alilipwa senti 75 nyingine kwa mzunguko mwengine wa vishimo 9. Hivyo, baada ya kumaliza mzunguko wa jumla ya vishimo 18 na muda wa karibu masaa mawili hivi, i.e. kuanzia saa 10.00 jioni hadi saa 12.00 jioni, kedi anamaliza kazi na kurudi nyumbani akiwa na jumla ya Shilingi moja unusu mfukoni. Hizo zilikuwa ni fedha nyingi sana siku hizo ukilinganisha na ukweli kuwa kiwango cha chini cha mshahara wa mfanya kazi serikalini wakati huo kilikuwa si zaidi ya shilingi 50.00 kwa mwezi. Na ndio maana vijana wengi wa Kikwajuni waliweza sio tu kukabiliana na hali ngumu ya maisha iliyokuwa ikiwakumba wao binafsi, lakini, vile vile waliweza kusaidia familia zao kwa kiasi fulani badala ya kutegemea kila kitu kutoka kwa wazee wao.

Ni nani hasa Chaap; alizaliwa wapi, lini na anafanya nini hivi sasa katika maisha yake?

Issa Mohammed Faki Mjaka ”Chaap” alizaliwa tarehe 10 Julai 1951 katika mtaa wa Kikwajuni. Alikuwa mtoto wa pili katika familia ya watoto saba (ikiwa wanaume watano na wanawake wawili) wa Bwana Mohammed Faki Mjaka na Bibi Mwantatu Issa Khamis. Alipata elimu ya msingi katika Skuli ya Msingi ya Holmwood (sasa Kidongo-Chekundu) kuanzia mwaka 1958 hadi mwaka 1966. Alimaliza masomo ya kidatu cha tatu katika Skuli ya Bububu. Alijiunga na Chuo cha Ufundi hapo Gulioni na kupata Shahada ya Ufundi wa Umeme. Mnamo mwaka 1976, Chaap aliajiriwa na Idara ya Habari na Utangazaji, Zanzibar kama Fundi wa Umeme.

'Chaap' akiwa katika mazoezi kwenye viwanja vya Golf, Maisara, mjini Zanzibar

Mnamo mwaka 1989 Issa Mohammed Chaap alibahatika kuhudhuria mafunzo ya Uenezi wa Habari katika Chuo cha Radio ya Cairo nchini Misri kwa muda wa miezi sita. Kutokana na kupenda kwake michezo, hasa mwanzoni mchezo wa Tennis, mnamo mwaka 1992, Chaap alipata fursa nyingine ya kuhudhuria masomo ya ukufunzi katika “University of Physical Education kama mwalimu “kocha” wa Tennis ya Meza (Table Tennis) huko Budapest nchini Hungary.

Mnamo mwaka 1995, Chaap alipata nafasi ya kushiriki katika mafunzo ya ukufunzi wa Tennis yaliyofadhiliwa na International Olympic Committee (IOC) yaliyofanyika Dar es Salaam katika viwanja vya Gymkhana. Vile vile, Chaap aliwahi kushiriki katika mafunzo kama hayo yaliyofanyika Arusha katika viwanja vya Gymkhana mwaka 2001. Lakini, ni katika mchezo wa Golf ambapo Chaap alipoonyesha kipaji chake na kupata mafinikio makubwa pamoja na umaarufu ndani na nje ya Zanzibar. Kutokana na umahiri mkubwa aliouonyesha katika michezo ya Tennis na Golf, Mwalimu wake wa kwanza aliyejuulikana kwa jina la Shashi alimuelezea Issa kama ni mchezaji “sharp” kwa jinsi alivyoimudu michezo hiyo miwili kwa wakati mmoja. Na hivyo ndivyo alivyojipatia jina la umaarufu “Chaap”, kwa maana ya kuwa alikuwa mwepesi kufahamu kila mbinu ya michezo hiyo na kuzitekeleza ipasavyo.

Anasimulia: “Nilianza kuupenda mchezo wa Golf mnamo mwaka 1962 nilipokuwa nawabebea Wakoloni wa Kiingereza mikoba yao iliyojaa vingowe vya kuchezea mchezo huo. Mimi, kama ilivyokuwa kwa watoto wengi wa Kikwajuni, nilifaidika sana na jinsi nilivyokuwa nikiona Wazungu hao walivyokuwa wanaucheza mchezo huo. Na ndipo nilipojifunza sheria na kanuni zake. Isitoshe, kibarua changu hicho kiliniwezesha kufahamiana na akina Sir George Mooring, Biles, Francis, Dulton na Wazungu wengi wengineo waliokuwa na daraja kubwa serikalini wakati huo. Kwa kweli, wao ndio waliokuwa wa kwanza kunijuulisha mimi na mchezo wa Golf. Na hivyo, nilipata bahati ya kujuana na kukutana nao nikiwa kedi wao”.

Issa Mjaka aliendelea kusimulia kuwa kazi ya ukedi aliendelea nayo mpaka yalipofanyika Mapinduzi ya Zanzibar mnamo mwaka 1964. Na baada ya hapo ndipo kedi wengi walipopata nafasi ya kutumia ujuzi na uzoefu walioupata kama kedi kuucheza mchezo huo katika kiwanja kile kile walichokuwa wakiwabebea Wazungu mikoba yao va Golf. Mwaka huo huo wa 1964 kulianzishwa “Mashindano ya Kedi” yaliyokuwa yakifanyika mara moja kwa mwaka. Akiwa na umri wa miaka 15, Chaap aliweza kutwaa ushindi wa kwanza mwaka 1964; na alitwaa ushindi wa pili mwaka 1965.

Miongoni mwa kedi na baadaye wachezaji wenzake kwa wakati huo walikuwemo Rajab Piru, Khamis Ramadhan, Khamis Shaaban, Shaaban Haroub, Mwinjuma Mzee “Jeff”, Hemed Mjaka, kaka yake Chaap, na Kombo Amir. Katika miaka hiyo ya awali ya uchezaji wake Golf, Mwalimu (coach) wao alikuwa Bwana Suleiman Mrisho “Kabalo” ambaye ndiye aliyekuwa mchezaji bora (Best Golfer) wakati huo na mchezaji mashuhuri wa mpira wa miguu wa timu za Kikwajuni na Taifa ya Zanzibar.

Akionesha kusikitishwa kwake, Chaap alisema kwa huzuni kuwa ilipofika mwaka 1967 mchezo wa Golf nchini Zanzibar ulianza kufa kidogo kidogo kutokana na kuanza kujengwa majumba na barabara ndani ya viwanja vya mchezo huo pale Maisara; na Furaha ya Visiwani Hoteli kujinyakulia rasmi viwanja pamoja na Golf Club iliyokuwa ikitumiwa na Wazungu hapo Maisara. Baada ya hapo, mchezo huo haukuchezwa tena mpaka mwaka 1982 katika viwanja vya Mnazi-Mmoja badala ya viwanja vya Maisara. Ingawaje viwanja vya Mnazi-Mmoja havikuanzishwa kwa madhumuni ya kuchezea Golf; lakini akina Chaap na wenziwe walijaribu kuvitengeneza ipasavyo ili kukidhi haja ya kuvitumia kwa mchezo huo ingawaje kwa muda mfupi.

Wakati huo, kedi wa zamani walijiundia timu yao ya kwanza kabisa ya mchezo huo ikiwa chini ya Uenyekiti wa Bwana Omar Ghassany. Hivi sasa, timu hiyo ya kedi wa zamani imepewa jina la “Maisara Golf Club” na ambayo ni timu pekee katika Zanzibar yenye wachezaji wa zamani wakishirikiana na wachezaji chipukizi. Jumla ya wachezaji pamoja na walimu/wachezaji wakongwe, kama vile Kabalo, Bushiri Mahmoud, Mkubwa Salum, Juma Saadat, Bwanakheri Omar na Ajar Patel katika timu hiyo haizidi wachezaji 25. Chaap mwenyewe ni mmoja kati ya walimu hao wanaowafundisha vijana chipukizi hivi sasa.

Hata hivyo, baada ya kufanyiwa matengenezo makubwa viwanja vya Golf vya Maisara, wachezaji walilazimika kuacha kuvitumia viwanja vya Mnazi-Mmoja na kurejea katika viwanja vya Maisara kwa ajili ya kufanyia mazoezi yao ya kila siku. Hivyo, walilazimika kurejea katika viwanja vya Maisara. Lakini, viwanja hivyo navyo vimevamiwa sana na wachezaji wa mpira wa miguu. Matokeo yake, wachezaji wa Golf wamefanikiwa kupata kutumia viwanja hivyo kwa mazoezi mara mbili tu kwa wiki; yaani kila Jumamosi na Jumapili, tena kuanzia saa 6 mchana mpaka saa tisa joini.

Haya ni mazingira magumu sana kwa kufanyia mazoezi ya mchezo wa Golf; mchezo ambao unahitaji kutumia akili na kupata utulivu wa kufikiri katika kila hatua ya uchezaji wake. Baya zaidi ni kuwa badala ya kutimiza ngwe ya vishimo 18 kwa ukamilifu wake, wachezaji wanapata fursa ya kucheza vishimo sita tu na kulazimika kurudia-rudia mara tatu ili wapate kukamilisha ngwe kamili ya vishimo 18. Hali hii inawakosesha wachezaji fursa ya kujipanua zaidi kimasafa na uwezo wa kutafakari juu ya kutumia vingowe vipasavyo kwa mujibu wa masafa na pahala unapotua mpira kila baada ya “shot” moja.

Nilipomuuliza Chaap kuhusu suala la vifaa vya kuchezea, kama vile mikoba na vingowe vyake, mavazi na viatu mahsusi vya kuchezea hasa ikitiliwa maanani kuwa vifaa vyote hivyo ni ghali sana; Bwana Issa, bila ya kufikiri sana alisema kuwa yeye pamoja na wachezaji wenzake wamekuwa wakiagizia vifaa vilivyotumika kutoka nje ya nchi kwa marafiki na wapenzi wengine wa mchezo huo. Bahati mbaya, mpaka sasa hawajapata wafadhili wa kutosha katika kusaidia kuuendeleza mchezo huo kutokana na ukweli kuwa Zanzibar haina hata kiwanja rasmi cha kuchezea mchezo huo. “Huwezi kumuomba mfadhili kusaidia chochote katika kukuza mchezo wa Golf nchini Zanzibar wakati mchezo huo si miongoni mwa michezo inayopendwa na wananchi wengi na wala uendelezaji wake haukupewa kipa-umbele na serikali”, alisema Chaap kwa masikitiko makubwa.

Hata hivyo, Chaap alifahamisha kuwa kutokana na mapenzi au utashi wa mtu binafsi tu kusaidia chochote katika kuendeleza mchezo huo, baadhi ya watu wamejitokeza kusaidia. Alisema, kwa mfano, Bwana Muzzamil yeye binafsi amekuwa akisaidia kwa kutoa fedha taslim na vifaa kwa ajili ya kuuendeleza mchezo wa Golf nchini. Chaap alifahamisha kuwa Bwana Muzzamil aliwahi kutoa jumla ya Shs. 70,000/- ikiwa ni nauli ya safari ya timu kwenda kushiriki katika mashindano huko Tanzania Bara.

Vile vile, Bwana Anthony Njoroge, ambaye ni mmiliki wa duka linalouza vinyago hapa Zanzibar, ambaye pia ni mpenzi na mchezaji wa Golf, aliwahi kutoa msaada wa fedha taslimu kulipia gharama za usafiri, malazi, ada za ushiriki pamoja na posho za wachezaji wa timu ya Zanzibar iliyoshiriki katika mashindano yaliyofanyika katika viwanja vya Gymkhana, Dar es Salaam hivi karibuni. Bwana Issa ametumia fursa hii kuwapongeza Bwana Muzzamil kwa msaada wao huo na hapo hapo kuwaomba wafadhili wengine wajitokeze katika jitihada za kusaidia kuuendeleza mchezo huo.

Kwa upande mwingine, ni jambo la kutia moyo kidogo kuona kuwa serikali imetenga fungu la fedha la jumla ya Shs. 800,000 tu kwa mwaka kupitia Baraza la Michezo la Zanzibar na chama cha “Zanzibar Golf Association” kilichosajiliwa rasmi mnamo mwaka 1982 na ambacho Mwenyekiti wake ni Bwana Mkubwa Salum, alieleza Chaap. Lakini, aliongeza kusema kuwa, inasikitisha sana kuona kuwa fungu hilo huwa linatolewa kimaandishi tu kwani gharama wanazozipata wachezaji wenyewe binafsi kila pale wanapolazimika kushiriki katika mashindano mbali mbali ya mchezo huo yanayofanyika ndani na nje ya Zanzibar ni kubwa zaidi ya kile kilichotengwa kwa ajili hiyo.

Kwa mfano, timu inapaswa kushiriki katika mashindano matatu kila mwaka yanayofanyika hapa nchini kama hivi: January – “Mapinduzi Cup”; September – “Maisara Open” na Desember – “Mkubwa Salum Cup”. Isitoshe, katika kipindi cha mwaka huu, timu imeshiriki katika mashindano ya “Arusha Open” ambayo hufanyika kila mwezi wa January kule Arusha na Zanzibar ilitoa wachezaji chipukizi (junior) 2 na mchezaji mzoefu (senior) 1. Katika mashindano hayo, jumla ya timu sita zilishiriki.

Katika mashindano ya “Morogoro Open” yaliyofanyika mwezi January 2010, Chaap alishiriki kikamilifu na kuchukua ushindi wa pili. Jumla ya wachezaji 4 kutoka Zanzibar walishiriki katika mashindano hayo ikiwa ni pamoja na Mussa Foum, Zehai Nassor na Abdul Nassir Ahmed; hawa wawili wa mwisho wakiwa wachezaji chipukizi. Juma Saadat alikuwa ndio Mwalimu (kocha) wa wachezaji hao katika mashindano hayo. Kutokana na ushindi wake huo, Chaap alizawadiwa kikombe pamoja na jiko la gesi (Gas cooker). Ukiacha mashindano hayo, wachezaji wa Zanzibar hushiriki kikamilifu katika mashindano mbali mbali yanayoandaliwa na Tanzania Golf Union (TGU).

Jee, kuna mashirikiano yoyote yale baina ya “Zanzibar Golf Association” na “Tanzania Golf Union”? Chaap alijibu suala hili kwa kusema kuwa mashirikiano baina ya vyama viwili hivi yapo na yanaendelea vizuri. Alieleza kuwa Mwenyekiti wa TGU, Bwana Bioniz Malinzi amekuwa akitoa msaada wake binafsi na kuhakikisha kuwa ZGA inapata mialiko ya kuhudhuria mashindano mbali mbali yanayofanyika Bara na kutoa basi maalum kwa ajili ya kuwasafirisha wachezaji kutoka Zanzibar. Hata hivyo, Bwana Issa Mjaka anashauri na kupendekeza kuwa kuna haja kubwa ya kukuza zaidi mashirikiano baina ya pande hizi mbili ili kwa pamoja mchezo wa Golf uweze kupata wachezaji, washabiki na wafadhili wengi zaidi kuliko vile ilivyo hivi sasa.

Nilimuuliza Chaap kwa madhumuni ya kutaka kujua ni nani hasa mchezaji bora wa Golf kupita wote nchini Zanzibar? Bila ya kusita, alijibu: “Kwa sasa, mimi ni mchezaji bora kuliko wote hapa Zanzibar. Inatosha tu kuangalia rekodi yangu na tunzo mbali mbali nilizozipata kutokana na kushiriki kwangu katika mashindano mbali mbali”.

Hata hivyo, Chaap aliongeza kuwa kwa upande wa wachezaji wazoefu (seniors), wachezaji bora wanaomfuatia yeye ni Juma Saadat na Mussa Foum. Na kwa upande wa wachezaji chipukizi (juniors), Chaap alitanabahisha kuwa Abdul Nassir Ahmed ambaye, mnamo mwaka 1999, alichukua ushindi wa kwanza katika mashindano ya wachezaji chipukizi ya “Lugalo Open” ndiye mchezaji bora katika ngazi hiyo kwa sasa.

Mwisho kabisa nilimuuliza Chaap iwapo anayo mapendekezo yoyote katika jitihada za kuukuza na kuuendeleza mchezo wa Golf nchini Zanzibar? Alijibu kwa kusema hivi: “Kwanza napendekeza kwa nguvu zake zote kwa serikali kuvirejesha viwanja vya Maisara kwa wachezaji wa Golf kupitia “Zanzibar Golf Association” ili tuweze kuvitumia kikamilifu kwa ajili ya kupata nafasi zaidi kwa mazoezi ya kila siku. Hii itatuondoshea kero zisizokwisha kutoka kwa wachezaji wa mpira wa miguu na madereva wa magari na vyombo vingine mbali mbali wanaoendelea kupita-pita viwanjani humo”.

Pili, kutokana na Golf kuwa ni mchezo wa kihistoria kwa Zanzibar, Chaap anaamini kuwa “Ikiwa mchezo huu utapewa kipa-umbele na serikali, kwa kuanzisha miundo-mbinu yake mipya na kuboresha iliyopo sasa, serikali pamoja na wananchi kwa jumla wataweza kuingiza mapato makubwa katika uchumi wa nchi. Vile vile, watalii wengi, kihistoria, wanategemea kuwa Zanzibar ni nchi ambayo inayo mandhari mazuri kwa mchezo wa Golf; lakini, bahati mbaya wengi wao wanaendelea kuvunjikwa moyo kwa jinsi wanavyoikuta Zanzibar katika hali ya kutokuwa na hata kiwanja kimoja cha kuchezea Golf”.

Chaap anamaliza kwa kusisitiza kama hivi: “Mchezo wa Golf ni maarufu sana duniani. Wachezaji maarufu kama vile Tiger Woods wametajirika sana na kupata umaarufu mkubwa katika ulimwengu wa Golf. Ikiwa jitihada za makusudi zitafanywa kwa madhumuni ya kuuendeleza mchezo huo hapa Zanzibar, basi hapana shaka yoyote kuwa vijana wengi ambao hivi sasa wanazurura ovyo kutokana na ukosefu wa ajira, wataweza kujituma na kujiajiri wao wenyewe kwa kushiriki kikamilifu katika mchezo huu. Ile dhana ya kuuona mchezo huo kuwa ni mchezo unaochezwa na matajiri tu ni potufu na imepitwa na wakati. Vijana pamoja na wazee/wastaafu wetu wanaweza kabisa kufaidika sana na fursa ambazo mchezo huu unaweza kuzitoa, iwe katika kuwapatia ajira vijana wetu au katika kuboresha afya za wazee wetu”.

Kwa hivyo, la muhimu zaidi, serikali inapaswa kuzingatia uwezekano au haja ya kuteua wajumbe wenye mapenzi na michezo mengine katika Baraza la Michezo badala ya kuendelea na uteuzi wa wajumbe wanaopendelea zaidi mchezo wa mpira wa miguu na mpira wa kikapu tu. Baraza la Michezo linapaswa kuwa ni baraza la michezo yote. Kwa kufanya hivyo tu ndipo uwakilishi wenye uwiano mzuri utakapopatikana na kuiwezesha serikali kutoa kipaumbele kwa michezo ambayo haina umaarufu au ushawishi mkubwa nchini ili iweze kujiendeleza ipasavyo. Kinyume chake, ikiwa serikali haitochukua hatua zipasazo, basi kuna hatari ya kupelekea kutoweka mchezo wa Golf kidogo kidogo na vijana wa Zanzibar kukosa fursa ya kurithishwa vipaji vya mchezo huo kutoka kwa wachezaji wakongwe ambao, kama ilivyokuwa kwa akina Sir George Mooring katika miaka ya 1960, itafika wakati nao watatoweka na kupotea kabisa.

Talib Kassim Abdi ni Mtafiti Msaidizi katika Taasisi ya Zanzibar inayoshughulikia masuala ya Utafiti wa Sera za Kimaendeleo na Kijamii (ZIRPP)). Hii ni makala yake ya kwanza tokea alipoanza kazi katika taasisi hiyo mapema mwaka huu.
talib.kweli@live.com

Advertisements

Actions

Information

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s
%d bloggers like this: