Serikali ya mpito au mbinu mpya ya kutaka kuendelea kutawala?

10 02 2010

Wapendwa Wazanzibari,

Mengi yameandikwa na yanaendelea kuandikwa kuhusu “Maridhiano” yanayoelezwa kuwa yamefikiwa baina ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Amani Karume na Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Shariff; maridhiano ambayo hayakubainishwa kwa kauli ya mdomo na wala hayakuandikwa popote pale. Katika kuelezea kutoridhika kwangu na hali ya usiri na ukimwa inayoendelea kuyakumba hayo maridhiano yanayozungumziwa hapa, niliwahi kumuomba Maalim Seif Shariff katika kikao cha Kongomano lililofanyika hivi karibuni katika Hoteli ya Bwawani atuwekee wazi nini hasa kilichozungumzwa na kukubaliwa kati yake na Rais Amani Karume. Alicheka tu bila ya kusema lolote. Baadaye nilifahamishwa kuwa ili maridhiano hayo yaweze kutekelezwa, kulikuwa na haja kubwa ya kuiwacha hali ya ukimya na usiri kuendelea.

Hivi karibuni tumekuwa tukishuhudia pendekezo kutoka vyama vya upinzani na jumuiya za kidini la kutaka uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu uakhirishwe hadi mwaka 2012; na shinikizo baada ya shinikizo linalomtaka Amani akubali kuongozewa muda wa kutawala, sio kwa kipindi kingine cha miaka mitano, bali kwa miaka miwili ya ziada akiwa ni kiongozi wa serikali ya mpito kuelekea katika uchaguzi ujao.

Katika hotuba yake aliyoitoa kule Pemba katika sherehe za kuadhimisha miaka 46 ya Mapinduzi ya Zanzibar, Amani alisema kuwa hatagombea kipindi cha tatu cha urais na huku akisisitiza haja ya kulinda na kutetea katiba ya Zanzibar ambayo inamzuia kugombea tena urais wa Zanzibar.

Lakini, kauli yake hiyo haimaanishi hata kidogo kuwa hayuko tayari kuiongoza Zanzibar kwa kipindi cha miaka miwili kama kiongozi wa serikali ya mpito kuelekea katika uchaguzi ujao. Na hii ndiyo hasa hoja ya Maalim Seif. Na, kwa hivyo, mpaka hapo Amani atakapoweka wazi kuwa hana dhamira ya kuiongoza serikali ya mpito hata kwa siku moja, basi tetesi zitabaki pale pale kuwa Amani hatagombea kipindi cha tatu cha urais, lakini inawezekana kabisa akakubali kuiongoza serikali ya mpito kwa muda wa miaka miwili ikiwa Baraza la Wawakilishi litapitisha azimio la kuakhirisha uchaguzi mkuu wa mwaka huu na kumtaka yeye kuiongoza serikali ya mpito kuelekea katika uchaguzi ujao; mamlaka ambayo wawakilishi wetu wanayo kwa mujibu wa katiba ya Zanzibar na kanuni za Baraza la Wawakilishi. Kelele za akina Msekwa, Makamba na wengineo ni za wapangaji tu; haziwakoseshi usingizi wenye nyumba.

Lakini, nini hasa madhumuni ya kuwa na serikali ya mpito? Ni jambo la kawaida kabisa kuwa serikali ya mpito huasisiwa kila pale inapotokea migogoro ya kisiasa au hali ya dharura katika nchi. Hatuna haja ya kwenda mbali kujifunza mifano iliyo hai na iliyowahi kutokea ili kupata maana halisi ya serikali ya mpito. Kwa mfano, baada ya kujiuzulu kwa Alhaj Aboud Jumbe mnamo mwezi April 1984, Ali Hassan Mwinyi aliteuliwa na Halmashauri Kuu ya CCM kuziba pengo lililoachwa wazi na Jumbe na kuongoza Serikali ya mpito kwa muda wa karibu miezi mitatu hadi uchaguzi ulipofanyika na Mwinyi kuchaguliwa rasmi kama Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

Isitoshe, serikali ya mpito pia iliwahi kuundwa nchini South Afrika baada ya kujiuzulu kwa Rais Tabho Mbeki; na Bunge la nchi hiyo kupitisha azimio la kumteua Bwana….kushika nafasi ya Mbeki mpaka hapo uchaguzi Mkuu ulipofanyika mwaka jana na Rais Jacob Zuma kuchaguliwa rasmi kuiongoza South Afrika kwa kipindi cha muda wa miaka mitano. Hali kama hiyo ilitokea nchini Liberia baada ya kujiuzulu kwa aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Charles Taylor, na nafasi yake kushikiliwa kwa muda wa mwaka mmoja na Bwana….ambaye aliongoza serikali ya mpito mpaka uchaguzi ulipofanyika na kuchaguliwa Bibi Ellen Johnson-Sirlief mwanamke wa kwanza kabisa kushikilia nafasi ya urais katika Bara la Afrika.

Kwa hivyo, kama tuonavyo hapo juu, serikali zote hizo za mpito ziliundwa baada ya kutokea migogoro ya kisiasa au dharura za aina fulani katika nchi hizo husika. Kwa upande wa Zanzibar, kujiuzulu kwa Jumbe kulisababishwa na “kuchafuka kwa hali ya hewa” na hivyo kusababisha kulazimika kujiuzulu kwake nafasi zote alizokuwa nazo ikiwa ni pamoja na urais wa Zanzibar. Nchini South Afrika, kujiuzulu kwa Mbeki mwaka mmoja tu kabla ya kumalizika kwa muda wake wa urais kulililazimisha Bunge la nchi hiyo kumteua rais wa muda kushika nafasi hiyo kwa sababu nchi haiwezi kujiendesha bila ya kiongozi. Hiyo ilikuwa ni dharura kubwa ambayo isingeliweza kuachwa bila ya kushughulikiwa ipasavyo. Halikadhalika, nchini Liberia mambo yalikuwa kama ilivyofanyika nchini Afrika ya Kusini. Liberia ilihitaji kupata kuiongozi wa muda mpaka uchaguzi utakapofanyika kutokana na kujiuzulu kwa rais wake kabla ya kumaliza muda wake. Hiyo nayo ilikuwa ni dharura kubwa ambayo iliikuta Liberia katika hali ya mgogoro wa kisiasa.

Sasa, tukirudi nchini kwetu Zanzibar; hivi kweli kuna haja ya kuundwa kwa serikali ya mpito? Nauliza hivi kwa sababu hakuna dharura au mgogoro wa kisiasa unaomlazimisha Rais Amani Karume kuachia ngazi kabla ya muda wake kumalizika. Hili la kwanza. Lakini, la pili ni kuwa ikiwa hoja inayojengwa hapa ya kutaka kuakhirisha uchaguzi ujao kwa madhumuni ya kumpa rais Karume muda wa kutosha ili kuhakikisha kuwa uchaguzi ujao unafanyika kwa misingi ya uhuru na haki na hasa zaidi kuondokana na siasa za uhasama na chuki na kupandikiza siasa za ushindani inakubalika, la kujiuliza ni kwanini muda huo uwe miaka miwili badala ya kutekeleza yote hayo katika kipindi chote kilichobakia cha urais wake? Ikiwa kweli Rais Karume ana nia ya kufanya hivyo, mimi ninaamini kabisa kuwa anaweza kurekebisha kasoro zote zilizojitokeza katika uandikishaji wa wapiga kura katika Daftari la Kudumu la Wapiga kura na pia kuhakikisha kuwa kila mwenye sifa za kupewa kitambulisho cha Uzanzibari anapewa mnamo muda huo huo uliobaki wa urais wake. Kwa lugha nyepesi, sioni sababu ya kuamini kuwa Serikali au Tume ya Uchaguzi inahitaji miaka miwili ya ziada kukamilisha zoezi la kuandikisha jumla ya wapiga kura wasiozidi 500,000 na ushei nchini kote.

Isitoshe, hivyo kweli Amani hana muda wa kutekeleza hayo maridhiano kati ya sasa hivi na mwezi Oktoba 2010? Na ni maridhiano gani hasa yanayozungumziwa hapa ambayo bado yanaendelea kuwa ni siri?
Na ikiwa kweli kuna haja ya kutekeleza maridhiano, kwanini lazima awe yeye wa kutekeleza maridhiano hayo na si mtu mwingine? Kwa kuendelea kuiongoza Zanzibar kwa muda wa miaka miwili mingine baada ya kumaliza vipindi viwili vya uongozi wake, Amani Karume haoni kuwa
ataonekana kuwa anataka kujiongezea muda wa kutawala kwa mlango wa nyuma; na hivyo kuweka mfano mbaya kwa viongozi wajao ambao nao pia wataweza kabisa kujenga mazingira yanayofanana na hayo; ilimradi tu wapate fursa ya kujiongezea muda wa kutawala kinyume na katiba ya nchi? Na ikiwa hili litaruhusiwa kufanyika, hivi Zanzibar itakuwa inaelekea wapi? Kuna haja gani, kwa hivyo, kuwa na katiba ya nchi ambayo haithaminiwi na wala kutekelezwa ipasavyo?

Kwa upande mwingine, ikiwa Maalim Seif na CUF watashiriki kikamilifu katika kuunda hiyo serikali ya mpito kama inavyotarajiwa, hapana shaka yoyote kuwa nao watajiwekea mazingira mazuri katika uchaguzi ujao kuliko wagombea wengine kutoka katika vyama vingine. Hii inatokana na ukweli kuwa yeye ni mgombea mtarajiwa wa urais wa Zanzibar kupitia chama cha CUF, wakati Amani hatokuwa mgombea tena. Serikali ya mpito ndiyo itakayoweka hayo “mazingira” mazuri yatakayohakikisha kuwa uchaguzi ujao utakuwa huru na wa haki.

Ikiwa dhana ya serikali ya mpito ni kuweka mazingira mazuri kwa kufanyika uchaguzi ulio huru na wa haki, kushiriki kwa Maalim Seif katika serikali hiyo kutaonekana kama ni “conflict of interest situation” kwa upande wake. Kwa maana nyingine, huwezi kuongoza serikali inayopaswa kuandaa uchaguzi ulio huru na wa haki na papo hapo kiongozi wewe ukawa ndio mmoja katika wagombea uongozi wa nchi katika uchaguzi unaotayarisha kufanyika. Hiki ndicho kilio cha CUF cha muda mrefu dhidi ya serikali inayoongozwa na CCM. Kitu gani kitatufanya kuamini kuwa Maalim Seif na viongozi wenzake watakuwa mara hii tofauti na viongozi wa CCM?

Kwa hivyo, ni vyema mtu mwingine ambaye atakuwa muadilifu kabisa kuiongoza hiyo serikali ya mpito. Rais Mstaafu Mwinyi angelikuwa kiongozi bora kushika nafasi hii ya muda; lakini haitowezekana kwa sababu mwanawe, Dr. Hussein Mwinyi, inasemekana kuwa ni mmoja wa wagombea watarajiwa wa urais wa Zanzibar. Vinginevyo, kumruhusu Mwinyi kushika wadhifa huo kuna uwezekano wa kuleta “conflict of interest situation” nyingine mpya. Kwa hivyo, mwanasiasa aliyebaki hapa, si mwingine, isipokuwa ni Salim Ahmed Salim. Yeye ni mtu bora kabisa kushika wadhifa huu wa muda kwa sababu hana azma wala dhamira ya kugombea urais wa Zanzibar.

Vinginevyo, jitihada hizi zote za kutaka kuakhirisha uchaguzi na kumtaka Amani kuongoza serikali ya mpito, zitakuwa si chochote zaidi ya mbinu ya kutaka kuendelea kutawala kwa mlango wa nyuma. Na hili kattu haliwezekani. Zanzibar haiwezi kujiwekea utaratibu mbaya ambao utaweza kutumiwa na viongozi wajao kila pale wanapotaka kujiongezea muda wa kutawala baada ya kumaliza vipindi vyao vya utawala kwa mujibu wa katiba. Ikiwa Amani Karume, kwa kuitumia CUF na Maalim Seif Shariff, ataruhusiwa na kufanikiwa kufanya hivyo, kitu gani kitawazuia wengine kufanya vivyo hivyo?


Muhammad Yussuf
Interim Executive Director
Zanzibar Institute for Research and Public Policy
P.O. Box 416
Zanzibar
TANZANIA
Tel: 0777 707820 Cellular
Tel: 0242 233526 Office
Email: yussufm@gmail.com
Weblog: http://www.zirppo.wordpress.com

Advertisements

Actions

Information

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s
%d bloggers like this: