Nani ana sauti ya mwisho Zanzibar?

26 11 2009

MWAFAKA wa kumaliza mtafaruku na vurugu za kisiasa visiwani Zanzibar uliofikiwa hivi karibuni baina ya Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Amani Karume na Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad sasa unaingia majaribu baada ya baadhi ya mawaziri kujitokeza hadharani kupinga uwezekano wa kuwepo Serikali ya Mseto.

Baada ya makubaliano, Maalim Seif aliwatangazia wafuasi wa CUF kwamba, chama hicho kimemtambua Karume kuwa Rais wa Zanzibar ili kumaliza mgogoro wa muda mrefu uliokuwepo baina ya pande hizo mbili na kurejesha amani na umoja wa Wazanzibari; hali ambayo ilitafsiriwa na baadhi ya wachambuzi wa kisiasa kuwa ni muelekeo wa kuwa na Serikali ya Mseto visiwani humo. Baadaye Karume alikiagiza chama cha CUF kumtumia majina ya watu wawili ili awape ujumbe wa mabaraza ya wawakilishi tangu chama hicho kilipokataa.

Wiki iliyopita Rais Karume alisema suala la kuwa na Serikali ya Mseto liko mikononi mwa Wazanzibari; kauli ambayo ilizua mjadala mkali huku baadhi ya watu wakisema CUF imeingia mkenge kama ilivyotokea huko nyuma. Mengi yamesemwa kuhusu mashaka yaliyopo juu ya makubaliano ya Karume na Seif kuhusu suala hilo kwa sababu yamegubikwa na usiri mkubwa; huku Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibarahim Lipumba akionyesha mashaka kwamba, huenda wameingizwa mkenge kwa sababu makubaliano hayo yalifanyika kwa mdomo (hayakuandikwa popote).

Wakati watu wakitafakari juu ya hali itakavyokuwa kwa Wazanzibari na hasa CUF wakiota kupata Serikali ya Mseto mwakani kama ushindani utakuwa kama miaka yote, wameibuka mawaziri wawili mmoja wa SMZ na mwingine wa muungano, ambao kwa nyakati tofauti walisema hadharani kwamba, Serikali ya mseto si muhimu visiwani humo.

Juzi Naibu Waziri Kiongozi , Ali Hassan Shamhuna na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Masuala ya Muungano), Sief Khatib ambaye anatajwa kuwemo katika orodha ya wanaowania urais wa Zanzibar mwakani, walisema Zanzibar haihitaji Serikali ya mseto na kwamba hayo siyo maamuzi ya CCM.

Shamhuna ambaye pia ni Waziri wa Habari wa SMZ alisema Zanzibar haihitaji Serikali ya mseto wala ya Umoja wa Kitaifa; kinachotakiwa ni kujenga utamaduni wa kukubali matokeo ya uchaguzi kwa kushinda ama kushindwa. Hii inamaanisha kwamba, utaratibu wa sasa uendelee hata kama mshindi atapatikana kwa tofauti ya kura moja.

Naye Khatib aliwaambia Wazanzibari kisiwani Pemba katika mkutano wa hadhara kuwa umoja wa Wazanzibari hauhitaji kushirikishwa chama kingine chochote, kwa sababu CCM peke yake inaweza kuweka umoja na mshikamano kwa vile ndiyo sera ya chama hicho.

Kwa ujumla kauli hizo zinachanganya na kubainisha kwamba, SMZ na CCM hawakubaliani na yaliyofikiwa na kina Maalim Seif na Karume katika kutatua tatizo la mvutano uliopo visiwani humo ambao umesababisha kudorora kwa maendeleo katika baadhi ya maeneo na kuwepo uhasama baina ya wananchi wa visiwani uliosababishwa na tofauti za kisiasa.

Kama ambavyo jumuiya ya kimataifa imeridhishwa na hatua iliyofikiwa; tulidhani kuna kila sababu kwa viongozi wa serikali kuwa mstari wa mbele kusimamia suala hilo. Cha kushangaza ni kwamba, Naibu Waziri Kiongozi anapingana na Rais wake, ambaye alimteua katika wadhifa huo! Au anataka kutuambia kwamba, rais amemtuma kueleza hilo ili asionekane kigeugeu?

Kwa ujumla tumeshangazwa na tabia za viongozi wetu kutoheshimu itifaki katika kuyatolea maelezo mambo yaliyosemwa na viongozi wa juu yao. Tunashindwa kuelewa kuwa nani ni mkubwa na mipaka ya wasaidizi wa rais ni ipi? Haiwezekani katika nchi ambayo kuna mfumo rasmi wa uongozi, kila mtu aseme lake. Kwa ujumla rais anapotoa tamko, viongozi wengine hawawezi kusema tofauti hata kama wanapinga.

Chanzo: Mwananchi, 26 Nov. 2009

Advertisements

Actions

Information

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s
%d bloggers like this: