Nafasi ya Kiswahili katika Ulimwengu wa Utandawazi

22 10 2009

Na Abeid Poyo

PAMOJA na baadhi ya watu kuibeza lugha ya Kiswahili, harakati za wadau kuikuza lugha hiyo kitaifa na kimataifa zimepamba moto. Kitivo cha Sanaa na Sayansi za Jamii cha Chuo Kikuu Huria Tanzania kimeongeza idadi ya watetezi wa Kiswahili wanaoamini lugha hiyo inakidhi mahitaji ya kitaaluma na kimawasiliano ndani na nje ya Tanzania.

Mwezi ujao, kitivo hicho kupitia idara yake ya Lugha na Fasihi kimeandaa Tamasha la Sauti za Kiswahili (Tasaki) ambalo pamoja na mambo mengine linalenga kutoa fursa ya kumulika na kutafakari mabadiliko na maendeleo ya Kiswahili katika dunia ya utandawazi ili kuleta uhuru na maendeleo ya kweli. Wasomi wa lugha wanaeleza kuwa lugha ya Kiswahili ni miongoni mwa rasilimali wanazoweza kutumia Watanzania ili kufikia maendeleo ya kweli.

Hata hivyo, mfumo mpya wa kimaisha ujulikanao kwa jina la utandawazi umekuja na upepo mkali ambao kama juhudi za makusudi hazitochukuliwa, upo uwezekano wa Kiswahili kuzolewa na kutupwa baharini na upepo huo. Ili kukumbatia lugha na utamaduni wetu, yatupasa kujenga ukuta imara ambao hautatikisika kwa upepo wa utandawazi. Ukuta huo basi ndio Tasaki ya Chuo Kikuu Huria. Kupitia Tasaki sauti ya Kiswahili itasikika ndani ya nchi, Afrika Mashariki, Afrika na ulimwenguni kote; anabainisha Mwenyekiti wa Tamasha Hadija Jilala.

Jilala na hata wenzake waliobuni wazo la tamasha, moja ya sauti muhimu za Kiswahili zinazopaswa kupazwa hewani na bila shaka kutiliwa maanani na jamii, ni ukweli kuwa lugha hiyo kwa sasa ina sifa ya kutumika kitaaluma shuleni na hata vyuoni. Kuna kasumba imejengeka kuwa hatuwezi kwenda mbele bila Kiingereza au huwezi kuwa umesoma bila kujua Kiingereza. Kuna nchi kama Japan zimeendelea kwa kutumia lugha zao, anaonyesha udhaifu wa hoja ya wanaokipinga Kiswahili kutumika kama lugha ya kufundishia.

Wapo wanaosema Kiswahili hakijitoshelezi kimsamiati. Tunataka tuwatumie wanafunzi katika madaraja mbalimbali kama sekondari na vyuo vikuu kuthibitisha namna wanavyoweza kuitumia lugha hii na ikatumika shuleni kama lugha ya kufundishia, anafafanua zaidi. Anasema kuwa laiti Watanzania wangejua thamani ya Kiswahili, wangejivunia nayo badala ya kushabikia lugha za kigeni hususan Kiingereza ambayo kwa hali ilivyo imeshawafanya kuwa watumwa wa utamaduni wake.

Ukweli wa mambo kwa sasa ni kuwa Kiswahili kinachobezwa na baadhi ya watu wenye mitazamo na kasumba za kikoloni tayari kimeshavuka mipaka ya kitaifa. Ni lugha inayoshuhudia mageuzi na kupiga hatua kubwa katika nchi kadhaa duniani. Watu wengi wanajifunza Kiswahili na vyuo vingi vikiifundisha lugha hiyo; kujivunia lugha yetu na utamaduni wake, tuipe nafasi na dhima maalum katika Nyanja zote za elimu, siasa, uchumi na utamaduni, anaeleza.

Kwa mujibu wa Jilala, tamasha hilo la wiki moja la kitaaluma na burudani linalochagizwa na kauli mbiu ya “Nafasi ya Kiswahili katika Ulimwengu wa Utandawazi” linakusudiwa kutangaza, kueneza, kuendeleza na kuinua lugha ya Kiswahili na utamaduni wake ndani ya zama hizi za mfumo wa utandawazi uliotamalaki duniani. Katika wiki ya sauti ya Kiswahili kutafanyika makongamano, mashindano ya uandishi wa kazi za kubuni kwa shule za sekondari, vyuo vikuu na watunzi wasio wanafunzi, anataja baadhi ya shughuli zitakazofanyika katika tamasha.

Anaongeza: “Kutakuwepo maonyesho ya sanaa na utamaduni, mavazi ya Kiswahili, vyakula vya Kiswahili, majigambo, ngoma, taarab, maigizo, utambaji wa hadithi, muziki wa kizazi kipya na ghani za mashairi mbalimbali”.

Jilala anasema nyanja zitakazoguswa katika tamasha kupitia mashindano ya uandishi wa kazi za kubuni au mada za kitaaluma ni pamoja na elimu, demokrasia, utandawazi, siasa, sayansi na teknolojia, utamaduni, mazingira, sheria, jinsia, ajira, ujasiriamali, Ukimwi, unyanyasaji wa kijinsia, watoto wa mitaani na masuala mengineyo ya kijamii.

Chanzo: Mwananchi

Advertisements

Actions

Information

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s
%d bloggers like this: