Rasilimali nyingi za Zanzibar bado hazijavunwa

6 10 2009
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa ZIRPP, Muhammad Yussuf

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa ZIRPP, Muhammad Yussuf

Na Hawra Shamte

Jumuiya mpya isiyo ya kiserikali inayojulikana kama Taasisi ya Utafiti na Sera za Kijamii (Zanzibar Institute for Research and Public Policy-ZIRPP) imeanzishwa Zanzibar kwa madhumuni ya kuwajumuisha na kuwatumia wataalamu na wasomi wa Kizanzibari walioko ndani na nje ya nchi ili kuzipitia sera mbali mbali zinazobuniwa na kutekelezwa na Serikali kwa kuzifanyia utafiti wa kina na kuangalia jinsi ambavyo zinavyoweza kuwasaidia Wazanzibari na Zanzibar kwa jumla katika jitihada zao za pamoja za kujiletea maendeleo ya kweli na endelevu na kutoa mapendekezo serikalini kwa madhumuni ya kuboresha utekelezaji wake.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa ZIRPP, Muhammad Yussuf, anasema kwamba utafiti umegundua kwamba Zanzibar ina rasilimali kubwa ya watu, na hasa wasomi na wataalamu wa kila fani, lakini wengi wao wako nje ya nchi na hivyo kutoinufaisha Zanzibar moja kwa moja kwa michango ya kimawazo na hata kiutendaji. Kwa hivyo, taasisi hii ina lengo la kuwajumuisha Wazanzibari popote pale walipo kwa madhumuni ya kuwawezesha kuchangia kimawazo na kifikra katika jitihada za kujiletea maendeleo ya kweli.

“Hii ni taasisi ambayo msingi wake ni wanachama; hivyo Mzanzibari yeyote anaweza kujiunga kwa kujaza fomu maalumu ya ombi la uwanachama na kulipa ada ya uwanachama ambayo ni Sh.13,500/00 tu kwa mwaka kwa Mzanzibari aishiye ndani ya nchi (Tanzania); na kwa Wazanzibari wanaoishi nje ya nchi ya Tanzania wanapaswa kulipa Dola 135.00 kwa mwaka”.

Pamoja na ada ya uwanachama, Wazanzibari pia wanaombwa kutoa michango mbalimbali ya hiari ili kusaidia shughuli za uendeshaji wake katika wakati huu muhimu wa awali wa kuanzishwa kwake na kupata usajili rasmi tarehe 2 Aprili mwaka huu.

“Bado tunahitaji kukodi jengo letu wenyewe kwa madhumuni ya ofisi; tunahitaji rasilimali, wafanya kazi na vitendea kazi. Kwa hivyo, tunahitaji, kwa kiasi kikubwa, michango ya Wazanzibari. Hivi sasa tumo katika mchakato wa kusajili wanachama wengi zaidi ili tuweze kufanya shughuli zetu kwa ufanisi. Isitoshe, kwa vile kazi tunazozifanya ni za utafiti, tunahitaji vile vile watu wa kujitolea; Wazanzibari wenye uwezo wa kufanya utafiti katika masuala ya kijamii na kiuchumi ili baada ya utafiti wetu tuweze kutoa matokeo ambayo asaa yatasaidia kuiboresha Zanzibar kimaendeleo na kiuchumi,” anasema Yussuf.

Aidha, Yussuf anaweka bayana msukumo wa kuanzisha taasisi hiyo ambao pia umo katika dibaji ya hati ya ZIRPP kifungu cha kwanza kinachosema:

“Sisi Wazanzibari kwa kuwa tunafahamu uwezo tulionao wa kitaaluma na kiujuzi katika nyanja mbalimbali; na pia tunafahamu kwamba tumesheheni katika udadavuzi wa masuala ya kimataifa na kwa kufahamu kwamba endapo uzoefu na ujuzi wa Wazanzibari kwa umoja wao ni nyenzo muhimu sana kwa maendeleo ya Zanzibar; hivyo ni azma yetu kutumia uwezo tulionao kufanya utafiti katika masuala mbalimbali ya kijamii na kiuchumi ili matokeo yake yawasaidie wabunifu wa sera ili waweze kutunga sera nzuri na bora zaidi kwa ajili ya maendeleo ya Zanzibar.”

Akielezea mfano wa sera ambazo wataziangalia na kuangalia ni kwa kiasi gani zimewanufaisha wananchi, Yussuf anasema:

“Mara tu baada ya Mapinduzi ya mwaka 1964, ardhi ilitaifishwa na kugawanywa kwa wananchi kwa madhumuni ya kuondosha ukiritimba wa umilikaji wa ardhi kutoka mikononi mwa matajiri wachache. Baadhi ya wananchi katika maeneo husika walipewa eka tatu tatu za ardhi kwa madhumuni ya kuboresha hali zao kiuchumi. Sasa, tunataka kuangalia utekelezaji wa sera hii iwapo bado unaendelea; na ulisaidia kwa kiasi gani katika kuinua vipato vya hao wananchi waliobahatika kupewa eka tatu tatu za ardhi.

“Ingawa tunafahamu kwamba sera yoyote ina uzuri na ubaya wake; na bila shaka wapo watakaopata hasara kutokana na utekelezaji mzima wa sera hiyo; na pia wapo watakaopata faida. Lakini, cha msingi hapa ni kuwa sera nzuri ni ile inayonufaisha zaidi kuliko ile inayoleta hasara. Kwa hivyo, tutaangalia faida na hasara zilizotokana na sera mbalimbali, kama vile afya, elimu, mazingira na kadhalika. Mara tu baada ya kukamilisha kufanya utafiti na kupata matokeo, taasisi itawasilisha ripoti yake serikalini kwa madhumuni ya kuitaka kutekeleza mapendekezo yake. Matokeo ya ripoti yatawasaidia wabunifu na watungaji sera kugundua mapungufu yaliyojitokeza katika sera husika na kuzifanyia marekebisho yapasayo ili waweze kutunga sera nzuri na bora zaidi siku za mbele; au kuboresha zilizopo na hata kuzifuta kabisa sera zisizo na faida kwa wananchi”, anaeleza Yussuf.

“ZIRPP itakuwa inatoa mapendekezo kwa serikali baada ya utafiti wa kina; kwa mfano, sera A imewasiaidia vipi wananchi katika kuwaletea maendeleo ya kweli. Kwa lugha nyingine, taasisi itaipongeza serikali ikiwa wananchi wamefaidika na utekelezaji wa sera husika kwa madhumuni ya kufanya bora zaidi. Lakini, papo hapo, taasisi itaikosoa serikali kila pale ambapo serikali imekosea ili iweze kujirekebisha. Nia yetu ni njema, na tunashukuru kuona kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeipokea taasisi hii kwa mikono miwili. Ni matarajio yetu kwamba serikali itatupa ushirikiano kadri itakavyowezekana”.

Hata hivyo, Yussuf anafahamu kwamba kuna msukumo mkubwa wa kisiasa visiwani Zanzibar ambao huwafanya watu kutokuaminiana. Je, vipi taasisi hiyo itafanya kazi zake katika mazingira ya aina hiyo?

“Sisi si wanasiasa na wala tusingependa wanachama wetu kuleta malumbano ya kisiasa katika jukwaa la ZIRPP; azma yetu kubwa ni kuwasaidia Wazanzibari kwa kuhakikisha kwamba sera zinazobuniwa na kutekelezwa na Serikali zinaleta manufaa kwa Wazanzibari wote na kuinyanyua Zanzibar kiuchumi, kimaendeleo na kijamii,” anasema na kuongeza:
“Tusingependa kuegemea upande wowote ule wa kisiasa; kwani tunaamini kwamba Zanzibar ni moja na Wazanzibari ni wamoja. Kwa hivyo, ni sisi Wazanzibari kwa umoja wetu ndio tutakaoijenga Zanzibar. Lakini, ikiwa tutatengana na kuendekeza malumbano, chuki na uhasama miongoni mwetu, basi tutakuwa tunaielekeza Zanzibar pahala pabaya”.

Akiongeza, Yussuf anasema: “Mimi binafsi naamini kwa dhati kabisa kuwa Wazanzibari tunapaswa kwanza tuguswe sana na Uzanzibari wetu kwa sababu tumejaaliwa visiwa vyenye upekee na uhalisia vyenye rasilimali za kutosha; vina fukwe za bahari za kuvutia; ardhi yenye rutba; na zaidi ya yote, Wazanzibari wamekusanya tamaduni nyingi tofauti; na hivyo kuwafanya watu wenye silka zinazovutia mataifa mengine. Mathalan, tunaweza kuiuza Zanzibar kwa njia ya kutumia lugha ya Kiswahili tu; tunaweza kuiuza Zanzibar kwa chakula na manukato yanayopatikana nchini; na ndio maana Zanzibar inajuulikana kwa umaarufu wake kama “spice island”, yaani, kisiwa cha manukato”.

“Vile vile, tunaweza kuiuza Zanzibar kwa usanifu wake wa mji tu (mji mkongwe); tunaweza kuiuza Zanzibar kwa ustaarabu na ukarimu wa watu wake; halikadhalika, tunaweza kuiuza Zanzibar kwa weledi wa watu wake. Hizi zote ni rasilimali za Zanzibar ambazo bado hazijavunwa vyema,” anasema Yusuf.

Hata hivyo, Yussuf anakiri kwamba mazingira ya utendaji kazi Zanzibar ni magumu kutokana na kutiliana mashaka ya kisiasa; lakini, ana imani kuwa pamoja na mivutano yote waliyonayo Wazanzibari, bado wanajivunia Uzanzibari wao; na hilo ni vigumu kulibandua kutoka nyoyoni mwao.

“Tutatumia moyo huu wa uzalendo na mapenzi makubwa waliyonayo Wazanzibari kwa nchi yao kujaribu kuwaunganisha, kuwashauri waione mantiki ya kuacha malumbano ya kisiasa na kuendeleza siasa zenye maslahi kwa mustakabali wa Zanzibar,” anasema Yusuf.

Anasema Zanzibar ilitambulika katika medani za kimataifa karne nyingi zilizopita, na pia hata kimaendeleo Zanzibar ilikuwa mbele kuliko nchi nyingi za Kiafrika. Ni miongoni mwa nchi za mwanzo kabisa za Kiafrika kuwa na reli, umeme na televisheni ya rangi. Hata katika sera ya kuinua hali za wananchi wake, Zanzibar ilipiga hatua kubwa sana katika miaka ya nyuma kufuatia mapinduzi ya Zanzibar. Kwa mfano, Serikali iliwahamisha wananchi katika nyumba za mbavu za mbwa kwa kuwajengea nyumba za kisasa katika maeneo kadhaa ya Unguja na Pemba kama vile, Michenzani, Kilimani na Makunduchi kisiwani Unguja; na Mtemani na Mkoani kisiwani Pemba. Vile vile, Nyumba za vijiji za Kiembesamaki Unguja, Gombani Pemba na kwengineko zilijengwa na kutolewa kwa wananchi bila ya malipo.

Kadhalika, kule Amani, Unguja, kuna nyumba ya wazee wasiojiweza ambao walikuwa wakihudumiwa na serikali. Pamoja na yote hayo serikali imeandaa nyumba maalum ya kuhudimia watoto yatima pale Forodhani. Huduma za maji, afya na elimu kwa muda mrefu zilikuwa zikitolewa na serikali bila ya wananchi kuchangia chochote.

“Kwa hivyo, ziko sera zilizowanufaisha wananchi, lakini kwa bahati mbaya sera nyingi hazikuwa endelevu kwa sababu za kiuchumi; na hasa zaidi kutokana na kudorora kwa uchumi wa Zanzibar na hasa kutokana na kuanguka kwa kiasi kikubwa sana kwa bei ya zao la karafuu katika soko la dunia,” anasema Yussuf.

Ama kuhusu suala la vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi, Yussuf anasema kimsingi wananchi kupewa vitambulisho ni jambo la kawaida na ni zuri kabisa; lakini, kutumia zoezi la uandikishaji na utoaji wa vitambulisho kisiasa ni makosa kwa sababu kila Mzanzibari anayo haki ya kupatiwa kitambulisho ilimradi tu amethibitisha Uzanzibari na uraia wake. Isitoshe, serikali kutambua nguvu kazi yake ni jambo muhimu katika utekelezaji mzima wa mipango na mikakati ya kuleta maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa kwa wananchi wake wote bila ya kubagua.

SOURCE: MWANANCHI

Advertisements

Actions

Information

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s
%d bloggers like this: