Wanaowania urais Zanzibar wapigana vikumbo Bara

8 09 2009

Na Salma Said, Zanzibar na Patricia Kimeremeta

KAMPENI za kuwania urais wa Zanzibar mwaka 2010, zimeanza kupamba moto huku wagombea watatu wanaotajwa kugombea nafasi hiyo kuanza kupita katika mikoa kadhaa ya Tanzania Bara kuomba kuungwa mkono. Habari zilizopatikana zinaeleza kuwa wanasiasa hao ambao ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Mohammed Seif Khatib, Waziri Kiongozi wa Zanzibar, Shamsi Vuai Nahodha na Naibu Waziri wa Ushirikiano Afrika Mashariki, Mohammed Abood.

Kwa mujibu wa habari hizo, Khatib anapigiwa debe na baadhi ya viongozi wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), huku Nahodha akiungwa mkono na Waziri wa Maliasili na Utalii, Shamsa Mwangunga. Wiki hii Waziri Abood amedaiwa kufanya kampeni katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ambako alizungumza na wenyeviti wa CCM wa mikoa ya Iringa, Mbeya na Ruvuma.

Chanzo cha habari kimesema kuwa Mwangunga naye alikuwa kwenye ziara katika mikoa ya Ruvuma, Mbeya na Rukwa ambako pamoja na mambo mengine, alikuwa akizungumza na makada wa CCM na kuwaomba wamuunge mkono Nahodha mwakani.

Hata hivyo, wagombea wote wamekanusha taarifa hizo wakisema kuwa hazina ukweli. Khatib alisema hajui kampeni zozote zinazodaiwa kufanywa na UVCCM kumpigia debe na kwamba kuhusu yeye kuwania urais wa Zanzibar mwakani, hawezi kusema chochote sasa kwa sababu muda haujafika. Abood naye alisema: “Sina mawasiliano na wajumbe hao wa mikoa na kama mnataka watafuteni mpate taarifa zaidi, labda kuna watu wanataka kunichafua,”. Alisema hawezi kuzungumzia nia yake ya kuwania urais wa Zanzibar sasa kwa kuwa sera ya CCM imefunga milango ya kufanya hivyo kabla ya wakati. Mwangunga na Nahodha hawakupatikana jana kuzungumzia suala hilo baada ya simu zao za mkononi kutopatikana.

Lakini, habari kutoka ndani ya CCM zimeeleza kuwa kampeni hizo za kumrithi Rais Aman Abeid Karume, zimetawaliwa na ubaguzi uliojikita katika tofauti za maeneo wanakotoka wagombea. Ingawa wakati wa kuanza kujinadi haujafika, mikakati ya chini chini imekuwa ikifanyika na makada hao wa CCM huku wapambe wao wakitupiana vijembe.

Ubaguzi wa kijimbo katika siasa za Zanzibar ulichochewa na ripoti ya utafiti wa Kampuni ya Synovate iliyoonyesha kuwa aliyekuwa Waziri Kiongozi wa Zanzibar, Mohamed Gharib Bilal, ndiye anayemfuatia kwa karibu Maalim Seif Sharif Hamad wa CUF kumrithi Rais Karume atakayemaliza muda wake wa miaka 10 ya kuiongoza Zanzibar mwaka 2010. Watu kutoka Kusini na Kaskazini kisiwani Unguja ndani ya CCM wanaupinga utafiti huo kuwa si sahihi; huku kila mmoja akivutia upande wake kwamba mgombea wao ndiye anayefaa.

Hata hivyo, Bilal ambaye pia anatajwa kuwania nafasi hizo bado hajaanza kampeni za kuomba kura kwa makada wa CCM kwa upande wa Bara. Dk. Bilal, ambaye kabla ya kuwa Waziri Kiongozi katika miaka ya 1995 hadi 2000, alikuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ni majeruhi wa kisiasa baada ya kuachwa katika uteuzi wa CCM katika kinyang’anyiro cha Urais mwaka 2000 dhidi ya rais Karume. Wengine waliopambana na Karume wakati huo ni Abdisalam Issa Khatib na mwanamke pekee Amina Salum Ali.

Katika uchaguzi wa ndani wa CCM wa kumpata mgombea urais Zanzibar, Dk Bilal alipata kura 44, Khatib alipata kura 11, Karume alipata kura 9 na Amina Salum Ali alipata kura 4. Matokeo hayo yalipopelekwa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM, jina lililorejeshwa lilikuwa la Amani Karume. Katika uchaguzi wa mgombea wa urais wa mwaka 2005, Dk Bilal alijitokeza kwa mara nyingine tena kujaza fomu ya kugombea urais Zanzibar, jambo ambalo liliwashangaza wengi kutokana na kuonekana kuwa amekiuka utaratibu unaotambulika ndani ya CCM wa kumwachia Rais aliyepo madarakani kumaliza kipindi chake cha pili cha miaka mitano.

Kamati Kuu ya CCM Zanzibar ilimwomba Dk Bilal aliondoe jina lake ili kumpa heshima Rais aliyepo madarakani amalize ngwe yake; Dk Bilal alikataa na kusema uamuzi wa kuondosha jina lake ni vema ukafanywa na Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM na ndipo majina mawili, lake na la Rais Karume, yalipopelekwa Dodoma.

Kundi linalomuunga mkono Dk Bilal limebaki na msimamo wake kwamba wanaye mgombea wao; na chini kwa chini linaandaa mikakati ya kuhakikisha mgombea wao sasa anamrithi Rais Karume mwaka 2010. Inawezekana mvutano huu wa Rais Karume na Dk Bilal katika siasa ndio uliosababisha Karume katika kipindi chote cha uongozi wake kutomteua Dk. Bilal kushika nafasi yoyote serikalini.

Hata hivyo, wanaompinga Dk Bilal wanadai kuwa huyu akiwa kiongozi itakuwa kama sawa na kumrudisha madarakani rafiki yake Rais Mstaafu, Dk. Salmin Amour, ambaye aliwahi kutaka kipengele cha muda wa urais madarakani kibadilishwe kwa kuongezewa muda.

Wengine wanaotajwa kuwania nafasi hiyo ya urais Zanzibar ni Naibu Waziri Kiongozi Ali Juma Shamhuna, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Ali Mohamed Shein, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali wa SMZ, Mheshimiwa Haroun Ali Suleiman, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi na Balozi Ali Karume (kaka yake rais wa Zanzibar, Amani).

Chanzo: Mwananchi

Advertisements

Actions

Information

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s
%d bloggers like this: