SMZ yapambana na Marekani

3 09 2009

Na Mwinyi Saadallah

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), imesema uamuzi wa Marekani kuwazuia raia wake kutembelea kisiwa cha Pemba, si jambo la busara na kinaweza kuathiri hali ya uchumi visiwani humu.
Hayo yalielezwa jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Kiongozi, Hamza Hassan Juma kufuatia kauli ya nchi hiyo kuwa kuna uwezekano wa kutokea vurugu wakati huu wa kuandikisha wananchi katika daftari la kudumu la wapigakura.
Alisema kwa kuwa Zanzibar inategemea sekta ya utalii, kauli hiyo inaweza kuwatia wasiwasi wageni na ndio maana serikali imeamua kueleza ukweli juu ya hali ya usalama Zanzibar.
“Watu wa Zanzibar wanakufa kwa ahadi ya Mwenyezi Mungu na watu
hukusanyika misibani na kwenye sherehe na huondoka salama, tunasema taarifa ya Marekani ni ya uongo”, alisema Waziri Hamza.
Alieleza kwamba tangu Zanzibar kuingia katika mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992, hakuna mgeni hata mmoja aliyeuawa kwa vurugu za kisiasa.
Alieleza kwamba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeamua kusambaza taarifa yake juu ya hali ya usalama iliyopo kwa ofisi zote za mabalozi nchini kwa vile taarifa iliyotolewa na Marekani ni ya upotoshaji.
Alisema taarifa ya Marekani kwa raia wake inaweza kusababisha athari kubwa katika sekta ya uwekezaji na inaweza kusababisha wasije Zanzibar kufungua miradi yao.
“Kama wana ushahidi na mgeni au mtalii aliwahi kuguswa tangu kuanzishwa mfumo wa vyama vingi basi watupe, tamko lao limetuumiza kiuchumi,” alisema Waziri.
Alifahamisha ni jambo la kushangaza kuona tamko kama hilo linatolewa wakati ni siku chache tu tangu mabalozi wa Jumuiya ya Nchi za Ulaya na Marekani kukutana na Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume lakini hawakumueleza hali hiyo.
Alisema katika kikao hicho, Rais Karume aliwahimiza mabalozi kutumia diplomasia kushauriana na vyombo vingine pale wanapotafuta ukweli wa mambo.
Hata hivyo, alisema inashangaza kuona Marekani inakataza raia wake wasitembelee Pemba, wakati raia wa nchi hiyo wanatembelea maeneo yenye vurugu, ikiwemo Iraq na Afghanistan.
Alisema serikali imesitisha zoezi la uandikishaji wapiga kura baada ya nchi za Ulaya kudai kuna kasoro katika utoaji vitambulisho vya ukaazi na kutoa nafasi ya kushughulikiwa mapungufu yaliyoyaona na si kutokana na kuvurugika kwa hali ya usalama.
Katika tarifa yake kwa raia wa Marekani mwishoni mwa wiki iliyopita, Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo, ilisema kuna uwezekano mkubwa wa kutokea vurugu zinazohusiana na uchaguzi wakati huu wa uandikishaji wapiga kura Pemba.
Taarifa hiyo ilisema kuna vikosi vya ulinzi na usalama vimekuwa vikipelekwa Kaskazini Pemba hasa katika Wilaya ya Wete na Micheweni, ambapo zoezi hilo lilianza na baadaye kusimamishwa.
Kutokana na hofu hiyo, Marekani iliwataka raia wake wasiokuwa na safari za lazima kuacha kutembelea kisiwa hicho hadi Disemba 20, mwaka huu.

Chanzo: Nipashe, 3 Septemba 2009

Advertisements

Actions

Information

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s
%d bloggers like this: