Laiti Tungejifunza Kwa Lugha Zetu

26 08 2009

Chambi Chachage

JE, unakumbuka neno hili ‘Tujifunze Lugha Yetu’? Hilo ndilo lililokuwa jina la vitabu vya kiada tulivyovitumia kujifunza Kiswahili enzi za Ujamaa. Kwa hakika lilikuwa andiko la kizalendo.

Siku hizi kuna msisitizo mkubwa wa kujifunza kwa lugha ya kigeni. Na si kujifunza tu kwa lugha hiyo, bali pia kuitumia kufundishia.

Lo, shule za Kiingereza imekuwa biashara nono mno!

Wataalamu wa ‘nadharia ya baada ya ukoloni’, au postcolonial theory kama wanavyoiita kwa Kiingereza, wanadai lugha ya kikoloni si ya kigeni tena eti sasa ni lugha yetu maana tumechangia kwa kiasi kikubwa kuibadili na kuikuza.

Hata maneno ya Kiswahili kama ‘Safari’ na ‘Uhuru’ leo yapo kwenye Kamusi ya Kiingereza. Eti nayo yamekuwa maneno ya Kiingereza.

Naam ni kweli kabisa tumechangia – kwa lazima au hiari – kukiendeleza Kiingereza.

Tena Afrika inajivunia kuwa na waandishi mahiri wa lugha hiyo. Wapo Wole Soyinka, John Cortzee na Nardine Gordimer waliopata mpaka Tuzo ya Nobeli ya Fasihi kutokana na maandishi yao kwa Kiingereza. Pia kuna kina Chinua Achebe na Ngugi wa Thiong’o wavumao katika medani hiyo.

Kwa nini basi, wanahoji waumini wa Kiingereza, tusitumie lugha hiyo ya kitandawazi kufundishia kwenye ngazi zote za elimu nchini? Kwa nini tung’ang’anie kutumia Kiswahili na hata tudai kitumike kabisa kuanzia chekechea hadi chuo kikuu? Hatuoni kuwa tutapoteza fursa ya kutumia lugha inayotambulika zaidi duniani? Au hatutambui kuwa Kiingereza ndio lugha ya soko huria -chombo cha mawasiliano kwenye uchumi na biashara ya ushindani ulimwenguni?

Wakati mjadala huu mkali ukiendelea, juma lililopita tulibahatika kupata ujio wa mmoja wa waandishi waliotajwa hapo juu. Ngugi alikuja kwenye ‘Kongamano la 6 la Umajumui wa Afrika la Usomaji kwa Wote’.

Kaulimbiu ya Kongamano hilo lililofanyika Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam lilikuwa ‘Usomaji kwa ajili ya Kuleta Mageuzi na Maendeleo ya Kijamii na Kiuchumi.’

Mwandishi huyu alitumia fursa hii kutukumbusha umuhimu wa kutumia lugha zetu kutunza kumbukumbu na kukuza maarifa ya jamii zetu.

Katika mhadhara mkuu wa Kongamano hilo alioupa kichwa kinachoweza kutafsiriwa kama ‘Dhidi ya Ukabaila wa Lugha na Udarwini: Mazingira ya Kujenga Utamaduni wa Kusoma’, Ngugi alisisitiza umuhimu wa uelewa/kuelewa.

Hakika huwezi kuleta maendeleo ya kijamii bila kuvirithisha uelewa wa kisiasa, kiutamaduni na kiuchumi wa jamii hiyo vizazi vyake.

‘Je umeelewa?’ Hilo ndilo swali ambalo mama yake Ngugi alikuwa akimuuliza kila baada ya maelekezo aliyokuwa akimpa kila alipokuwa akimtuma kwa ndugu zake enzi za utoto wake. ‘Yule mzazi asiyewajibika tu’, anatukumbusha Ngugi, ‘ndiye anaweza kutoa maelekezo kwa kutumia maneno na lugha ambayo mtoto wake haielewi.’

Lakini hivyo ndivyo tunavyofanya kwa kuanza ghafla kufundishia kwa Kiingereza baada ya kufundishia kwa Kiswahili shuleni.

Tunafanya hivyo japo tunajua fika kuwa hatuna walimu wa kutosha wanaojua hata kufundisha Kiingereza kama lugha ya pili licha ya kukifundishia. Mfano wa kuaibisha kuhusu mkanganyiko huu ulitolewa hivi karibuni Bungeni na Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Gertrude Lwakatare.

Mbunge huyo alisema: “Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi mwenyewe ni shuhuda, nilienda kule kwetu, nilikuwa napita nikasikia Mwalimu anasema “this is a kinife” anamaanisha knife. Nikaingia darasani, kuingia darasani, nikamsaidia nikamwambia hii inatwa knife (“naifu”), usiseme “kinife”. Au mtoto wa Form Six anakwambia “my phone is crying”.

Your phone is not crying, is ringing! Ni kwa sababu ya vitu vidogo, kwa sababu hatuko fluent, tujitahidi, tusione aibu.” Wabunge wakacheka. Na kupiga makofi. Mjadala ukaisha. Sera ya lugha ikabaki vilevile.

Hili ni suala zito la kisera. Si jambo la kulifanyia mzaha. Wala kulichekea. Limetugharimu sana kama nchi. Na linatupoteza kama jamii. Ni kitu cha kustaajabisha.

Tena hakifanyiki katika nchi zingine. Eti kuwafundishia watoto kwa lugha wanayoielewa kwa miaka saba bila kuwafundisha vizuri lugha wasiyoielewa. Kisha kuanza ghafla kuwafundishia kwa lugha hiyo wasiyoielewa!

Laiti tungeweka pembeni kasumba na kutambua kuwa suala hili si suala la uzalendo tu.

Ni suala la ubinadamu. Unapomnyima mtu fursa ya kujifunza kwa lugha yake anayoitumia na kuielewa zaidi unamnyang’anya utu wake.

Tena unamwibia uhuru wake wa kufikiri, kuhoji na kuvumbua katika muktadha wa mazingira ya jamii yake. Unamfanya mtumwa katika nchi yake mwenyewe.

Ndio maana kuna umuhimu wa kuzitafakari kwa makini hoja alizozitoa Ngugi katika huo mhadhara wake. Na kuna hitaji la kuzingatia hoja kuu ya kitabu chake kipya cha ‘Re-membering Africa’.

Jina la kitabu hicho lina maana ya kuwa Afrika imevunjwavunjwa kwa ukoloni na ubeberu wa lugha za kigeni na inahitaji kuungwa tena kwa kutumia kumbukumbu za lugha zetu.

Tukitaka kuendeleza maarifa na kujiletea maendeleo yetu wenyewe tuenzi lugha zetu. Tujifunze lugha zetu. Tufundishe kwa lugha zetu. Tutafiti kwa lugha zetu. Tuvumbue kwa lugha zetu zote.

Kama anavyoghani Malenga ‘Issa Bin Mariam’:

Amkeni, Waafrika.

Uafrika ni Umajumui wa Afrika.

Oteni ndoto, Kizaramo,

Fikra, Kiswahili; mawazo Kigikuyu.

Chanzo: Mwananchi

Advertisements

Actions

Information

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s
%d bloggers like this: