Tunainasuaje Zanzibar katika mgando huu?

23 08 2009

Na Ally Saleh Hoja

SUALA uandikishaji wapiga kura hapa Zanzibar sasa linaanza kuchukua sura nyengine pale wiki iliyopita Serikali ya Zanzibar ilipojuburi tamko lililotolewa na Umoja wa Ulaya, Marekani na Japan lililosema na kutoa wito kuwa Serikali zinapaswa kuhakikisha kuwa Watanzania wote wanapata haki ya kujiandikisha katika daftari la wapigakura na kwamba SMZ iondoshe kasoro zilizojitokeza katika zoezi hilo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Kiongozi, Hamza Hassan Juma alisema si vyema kwa mabalozi kukaa Dar es Salaam na kutoa kauli na pia alijitutumua na kusema kuwa Zanzibar haitishwi wala haiongozwi na yeyote kwa sababu ni nchi huru na inayofuata katiba. Baya katika kauli ya Waziri Juma ni kuwa alikiri kuwa hajaliona tamko hilo wala hajakutana na mabalozi hao au japo mwakilishi wao ili afahamu wapi anasimamia katika maoni yake. Bila shaka Waziri Juma hakutaka aonekane yuko nyuma au anashindwa na jambo na ndipo akatoa kauli ambayo kwa fikra zangu ni ya bahati mbaya, isiyomstahikia na hata kuweza kuiweka pabaya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar mbele ya macho ya wafadhili.

Na hii si mara ya kwanza kwa wanasiasa wa Zanzibar kutoa kauli zinazofanana na hizo pale mabalozi wanapokosoa mwenendo fulani hapa Zanzibar hasa kuhusiana na siasa, utawala bora na haki za binadamu na hutokezea matamshi kama hayo kuwakera wanasiasa hao na kujikota wakiyasema yale yasiyostahili kusemwa. Naamini Waziri Juma anajua fika kuwa zama zimekwisha za kuamini kuwa nchi haiwezi kuhojiwa kwa dhulma dhidi ya wananchi, usimamizi mbovu wa haki zao au mtiririko mbaya wa kuhimiza demokrasia. Kwamba mipaka ya nchi ni kinga; ni jambo ambalo halipo tena.

Dunia hivi leo imekuwa ndogo sana na kwa udogo wake athari ya nchi moja inazifikia nchi nyengine nyingi na kuwa dunia imekubaliana kuwa lazima kuwe na viwango ambavyo kila taifa inafaa kuvifikia na wale wataoshindwa wakumbushwe, wahimizwe na hata wachukuliwe hatua. Nchi zetu yaani pamoja na Zanzibar zinajua hakika kuwa jumuia ya kimataifa inapenda kutuunga mkono katika harakati zetu za kujiimarisha kiuchumi na hivyo pia kimaendeleo lakini pia wangependa kuona utaratibu wa kidemokrasia unaimarishwa ili kuweza kuhakikisha uchumi na maendeleo yanadhibitiwa na kuwa endelevu.

Hatukatai kuwa hatua kubwa ya kidemokrasia imepigwa na ndio maana leo tuko hapa tulipo, lakini ni kosa kubwa kuamini kuwa kila kitu kimeshafanywa na zaidi kukasirika pale tunapoambiwa bado kuna nafasi ya kufanya mengine zaidi ili demokrasia yetu ipevuke. Waswahili husema tutazame mawili mawili, hivi kweli viongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ndani ya dhati yao, ndani kwenye vilango vya mioyo yao, wanaamini kuwa uandikishaji wa wapiga kura umekuwa ukienda sawasawa na kwamba uandikishaji wa vitambulisho vya Mzanzibari umekuwa ukienda sawa pia?

Hivyo kweli kelele zinazopigwa na Wapinzani na huu ushauri uliotolewa na Wafadhili haiwi ni zinduko kwa Serikali ya Zanzibar kuwa kuna dosari ambazo zinafaa zirekebishwe na zisiporekebishwa leo zitakuwa na athari kubwa huko mbele? Mimi sifahamu pale Waziri Juma anapopiga kifua kujuburi kauli ya Wafadhili anakusudia kuipa Zanzibar faida gani ya kisiasa au kuipinga kauli hiyo kutafuta ukweli kuwa undikishaji wapiga kura hadi sasa umeparaganywa? Ni fikra zangu kuwa matamshi hayo ya mabalozi bila ya shaka hata kama hatuyapendi kiasi gani lakini hayakuja bila ya kufanya utafiti na kawaida najua uandishi wa tamko lao umepitia uchunguzi mkubwa na namna bora ya kupanga kila neno katika tamko hilo.

Au ndio kama alivyotoa kauli kuwa Serikali haikusudii kushughulika hata iwapo watu watakaoandikishwa wakiwa kidogo basi bado Uchaguzi Mkuu hapo mwakani utakuwapo kwa maelezo tu kuwa ziko baadhi ya nchi ambazo wapiga huwa hawazidi asilimia 30 au 40? Naamini Waziri Hamza anajua kuwa wafadhili wanachangia nusu nzima ya gharama za mchakato mzima wa upigaji kura hapa Zanzibar ingawa nisieleweke kusema kwa hivyo wana haki ya kuingilia, ila sioni kuwa hawana haki ya kujua fedha zao zitaleta tija gani. Sifikiri wanaweza kuridhishwa na kauli kuwa kila nguvu itatumiwa kuhakisha kuwa uandikishaji unaendelea, au kauli kuwa kila mtu ameshapewa kitambulisho cha Mzanzibari, au itoshe tu kusema kuwa watu 8,000 hawajachukua vitambulisho vyao, au kujenga mazingira ya kwata za wanajeshi kuonekana njiani na vifaru kutinga barabarani.

Naamini Wafadhili wangependa kusikia kuwa hekima inatawala katika uandikishaji, hakuna jimbo litaloandikishwa bila ya utafiti na uhalisi wa kujulikana watu wenye vitambulisho vya Mzanzibari, kwamba masheha wanaolalamikiwa katika upatikanaji wa vitambulisho vya Mzanzibari wanatolewa katika mnyororo wa kazi hiyo ( kicked out of the equation) na kuwa masheha hao pia hawawi kipingamizi kwa watu wenye sifa kuingia katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. Wafadhili na wafuatiliaji wa nyenendo za demokrasia wasingependa kusikia pia kuwa wanafunzi wanaingizwa katika zogo hilo la uandikishaji, lakini wangetaka pia kuona kuwa wanafunzi waliotimiza masharti hawakosi haki ya ya kujiandikisha kuwa wapiga kura.

Binafsi fikra zangu ni kuwa kama Idara ya Vitambulisho ingekuwa imejipanga vema basi hakuna kundi rahisi kuliandikisha kama hili maana tunajua kuwa wanafunzi wetu wakifikia kidato fulani huwa wametimia miaka 18, na kama Idara hiyo ingeifanya kazi hiyo kuanzia 2006 hadi leo, basi kusingekuwa na zogo hili la sasa na wala madai ya wanasiasa ‘kuwachochea’ wananchi wadai vitambulisho. Mara nyingi sisi tunakuwa hodari wa kujiwekea kinga (defence) kuwa hali ya Zanzibar ni ya namna ya pekee, historia ya Zanzibar ni ya misukosuko ili kuzuia tusiambiwe tunavyofanya sivyo au kuelekezwa njia bora zaidi.

Tunaposema hali yetu ni ya pekee na historia yetu ya misukosuko lakini tunayafanya kama yanayofanywa na wengine katika kupigania vyama vyetu vibaki madarakani au hata kulinda maslahi ya kisiasa ya kundi fulani. Kwangu tatizo kubwa lilolizonga daftari hili ni kuwa vyama vinaamini kwamba kupata chama kimoja wapiga kura wengi na kingine kuandikishwa wachache ndio njia pekee ya kupata ushindi katika uchaguzi mkuu. Na hili halitatufikisha mbali kwa sababu inaelekea tuna uvivu wa kujenga mikakati zaidi ya kuhamasisha wapiga kura wetu wengi wanaingia katika daftari na wengi wanajitokeza kupiga kura na kutupigia kura.

Kama hilo hatutalifanyia kazi basi ni wazi kuwa tutagombana na Wafadhili na pia tutaendelea kugombana sisi kwa sisi, maana ni ukweli kuwa wapiga kura wetu ni hawa hawa wananchi wetu na kama kuna upande unaamini kuwa ushindi ni kwa kuwazuia wengine na upande mwengine unaamini kuwa ushindi ni kwa kuwazidi wengine, basi hatufiki mbali kwani tutakuwa tunanyang’anyiana mbao wakati huo jahazi tumeshalibomoa. Utakuja Uchaguzi Mkuu 2010, 2015 na mwengine na mwengine na sisi tutabaki katika malumbano ya vitambulisho, daftari, masheha na mambo madogo madogo na wakati huo Zanzibar ikinasa katika mgando na kujikuta haina nguvu katika mvutano wa kamba.

+255 777 4300 22

http://www.eternaltourszanzibar.net

jumbamaro.blogspot.com

Advertisements

Actions

Information

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s
%d bloggers like this: