SMZ yatangaza vita Pemba

23 08 2009

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imetangaza rasmi kutumia nguvu za dola kupambana na makundi ya watu wanaojihusisha na vitendo vya kigaidi katika Kisiwa cha Pemba. Msimamo huo ulitolewa jana na Waziri wa Nchi Afisi ya Waziri Kiongozi, Hamza Hassan Juma katika Ukumbi wa Karimjee, jijini Dar es Salaam wakati wa kongamano la siku moja, lililoandaliwa na Chama cha Wananchi (CUF) kwa lengo la kujadili hali ya kisiasa kisiwani Zanzibar. “Napenda kutoa msimamo wa SMZ juu ya vitendo hivi, kuanzia sasa tunasema tutatumia nguvu zote kushughulikia magaidi wa aina yoyote watakaojaribu kuvunja amani na utulivu uliopo… hatutawavulimia hata kidogo,” alisema Waziri Juma.

Alisema kwa vile serikali ipo kwa ajili ya kuwalinda wananchi wake, haitakubali kuona hali ya uvunjifu wa amani inachukua nafasi kubwa wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2010. “Suala la amani halipaswi kuchezewa hata kidogo, wananchi wetu wamekuwa wakipandikizwa chuki na wanasiasa ambao yakitokea matatizo utakuta hawapo, lakini wanaoumia ni hao hao wananchi,” alisema Waziri Juma.

Alisema kutokana na hali hiyo, SMZ inatoa tahadhari kali kwa wananchi ambao watagundulika kujiandikisha zaidi ya mara moja wakati wana vitambulisho. “Tunafanya utafiti juu ya suala hili na tukigundua vitambulisho vyao vipo na wanafanya vurugu za makusudi, tutawachukulia hatua kwa mujibu wa sheria, kwani wanasababisha wenzao kukosa haki zao na siasa ya Zanzibar kuonekana haifai, si kweli, siasa ya Zanzibar haiko kama inavyoelezwa,” alisema Waziri Juma.

Alisema suala la uandikishaji wananchi limegeuzwa kuwa la kisiasa zaidi kuliko hali halisi. Aliwataka wanasiasa visiwani kufanya kazi zao za siasa na si kuingia katika masuala ya kisheria.

Akichangia katika kongamano hilo, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willbrod Slaa, alimtupia lawama Rais Jakaya Kikwete kwa kusema amekuwa kimya mno tangu fujo hizo kutokea. Alisema historia itamhukumu Rais Kikwete kwa ukimya wake, kwa vile anaonekana wazi amebariki hali hiyo kuwepo katika Kisiwa cha Pemba. “Serikali yoyote inaposikia kelele au manung’uniko, jambo la kwanza ni kusikiliza na kusuluhisha na si kutumia ubabe… amani haiteremki kutoka mbinguni, inajengwa, hatutaki kuyaona tena ya mwaka 1995, 2000 na 2005 yanatokea, tunataka tufanye uchaguzi kwa amani tusitunishiane misuli,” alisema Dk. Slaa.

Kutokana na hali hiyo, Dk. Slaa aliitaka Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kukutana mara moja ili kujadili kasoro zilizojitokeza katika suala zima la uandikishaji na utoaji wa vitambulisho. “Tume hizi zinapaswa kukutana haraka kujadili kasoro zilizojitokeza ili kuepuka matatizo kama yale yaliyotokea Burundi na Rwanda… hatutaki kufika huko,” alisema Dk. Slaa.

Naye Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, alisema machafuko yanayotokea visiwani humo yanahusishwa moja kwa moja na Rais Kikwete kwa vile ameruhusu vikosi vya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na vifaru kupelekwa Pemba. “Yeye kama Amiri Jeshi Mkuu, anahusika katika hili, kwa sababu amebariki vifaru na askari wa JWTZ kupelekwa Pemba, utadhani kuna machafuko makubwa… huku ni kutisha wananchi, nawaambia historia itamhukumu,” alisema Maalim Seif. Alisema katika hali ya kushangaza, hakuna mwanachama hata mmoja wa CCM aliyenyimwa kitambulisho, kitendo ambacho kinadhihirisha wazi kuna mipango maalumu ya kudhoofisha upinzani.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Vitambulisho Zanzibar, Mohamed Juma Amme, aliwatuhumu wanasiasa kuwa wamekuwa wakichochea wananchi kufanya vurugu ili kuharibu zoezi la uandikishaji. “Suala hili ni dogo, lakini limekuzwa na wanasiasa wetu ili kupotosha hali halisi iliyopo, serikali ilifanya makusudi kutumia vitambulisho vya kura kwa maana nzuri tu, kuna vitambulisho zaidi ya 7,000 viko vituoni, lakini wananchi wamegoma kwenda kuvichukua, sasa nani wa kulaumiwa?” alihoji Amme. Alisema ofisi yake haitasita kuwafungulia mashitaka wanasiasa wanaotoa kauli za uchochezi bila ya kuwa na uthibitisho.

Kongamano hilo la siku moja, lililokuwa chini ya Uenyekiti wa Profesa Ibrahim Lipumba, lilikuwa na lengo la kujadili na kupata ufumbuzi wa athari za uandikishaji kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Zanzibar na matumizi mabaya ya vyombo vya dola. Baadhi ya viongozi wengine waliohudhuria kongamano hilo ni pamoja na Msuluhishi wa Mgogoro wa Darfur, Dk. Salim Ahmed, Salim, Waziri Mkuu mstaafu, Joseph Warioba, Brigedia Jenerali mstaafu Hashim Mbita, wabunge na viongozi wengine mbalimbali.

Chanzo: Tanzania Daima

Advertisements

Actions

Information

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s
%d bloggers like this: